1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado Haiti haijatengemaa

12 Januari 2011

Leo Haiti yatimiza mwaka mmoja tangu ikumbwe na tetemeko kubwa la ardhi hapo Januari 12, 2010, lakini bado hali ya mambo haijakaa sawa hadi sasa nchini humo, ambayo inakabiliwa pia na janga la kipindupindu na machafuko.

https://p.dw.com/p/zwgQ
Kipindupindu kingali kinawakabili Wahaiti
Kipindupindu kingali kinawakabili WahaitiPicha: AP

Bado Wahaiti wanakabiliwa na njaa, ukosefu wa makaazi mapya pamoja na ugonjwa wa kipindupindu. Watu wanasubiri pia matokeo ya uchaguzi wa duru ya kwanza wa Rais uliofanyika Novemba 28 mwaka 2010, ambao uhalali wake unaonekana kutiliwa shaka na Wahaiti wengi pamoja na waangalizi wa kimataifa, kutokana na udanganyifu na mapungufu mengine makubwa.

Hii ndiyo hali halisi ya Haiti leo hii inapozindua kumbukumbu ya mwaka mmoja baada ya tetemeko kubwa la ardhi , kwa kufanya kumbukumbu katika maeneo ya makaburi yaliyozikwa wahanga wa tetemeko hilo wakati viongozi wakitetea hatua za kimataifa zinazokosolewa za kuisaidia nchi hiyo na kuzindua mpango wenye matumaini wa uwekezaji nchini humo.

Mgombea urais wa Haiti, Jede Celestin
Mgombea urais wa Haiti, Jede CelestinPicha: picture-alliance/dpa

Akizindua siku mbili za kumbukumbu ya maafa ya tetemeko la ardhi la Januari 12, Rais Rene Preval ameweka shada la maua katika eneo la mlima ambalo lina makaburi hayo. makundi ya watu yanatarajiwa kuhudhuria misa ya kuwaombea watu waliopoteza maisha , misa itakayofanyika katika kanisa lililoharibiwa na tetemeko hilo katika mji mkuu Port-au-Prince mapema leo Jumatano.

Uchumi na miundo mbinu katika nchi hiyo imeharibika, mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaendelea kuuwa na zaidi ya watu 800,000 wanaishi katika makambi yaliyojengwa kwa mahema. Ujenzi mpya haujaanza kabisa.

Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton , mmoja wa watu maarufu wanaoratibu juhudi kubwa za misaada ya kimataifa , amewasili jana Jumanne kujiunga na kumbukumbu hiyo na amesema kuwa anavunjwa moyo na kasi ndogo mno ya ujenzi mpya wa makaazi ya watu. Pia ameitaka serikali kutatua mkwamo kuhusiana na uchaguzi.

Brian Concannon , ambaye amewahi kuwa mjumbe wa Marekani wa haki za binadamu , anaona kwamba suala kuu katika uchaguzi huo si kurejewa kuhesabiwa kwa kura , bali ni mapungufu makubwa katika hatua za uchaguzi huo.

Taarifa ya makundi ya waangalizi wa uchaguzi huo zinasema , kuwa wapiga kura wengi ambao walikuwa na vyeti vya kuwaruhusu kupiga kura, hawakuweza kupiga kura, kwasababu majina yao hayakuwapo kwenye orodha ya wapiga kura. Inakadiriwa kuwa karibu asilimia 10 ya Wahaiti hawakuweza kutambuliwa katika uchaguzi.

Mwandishi: Pontes, Nadia/ZR /Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf Saumu Ramadhani