1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Idadi ya maafa yafikia 150

8 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBkn

Idadi ya vifo kutokana na mashambulizi matatu ya hivi karibuni ya kujitolea muhanga maisha kwa kujiripuwa kaskazini mwa Iraq imeongezeka na kufikia watu 150.

Serikali ya jimbo la Tikrit imesema leo hii kwamba idadi ya watu waliojeruhiwa imefikia 200.Wizara ya Afya ya Iraq ilirepoti hapo awali kwamba idadi ya watu waliopoteza maisha yao kutokana na mashambulizi hayo yaliotokea Ijumaa jioni na mapema hapo jana ni watu 115 na kwamba wale waliojeruhiwa ni 205.

Lori liliotegwa bomu limeripuliwa katika soko lenye harakati kubwa katika mji wa kaskazini wa Tuz Khurmato ulioko katika jimbo la Tirkit ambao unakaliwa na watu wengi wa madhehebu ya Shia.

Akizungumna na waandishi wa habari walioko Washington Marekani kwa mawasiliano ya video kutoka Baghdad Meja Generali Rick Lynch kamanda wa majeshi ya muungano katikati ya Baghdad amesema kuondolewa kwa wananajeshi wa Marekani nchini humo wakati huu kutachochea machafuko.

Amesema wanaweza kukabidhi eneo hilo kwa wanajeshi wa ulinzi baada ya muda fulani na hapo wataweza kuchukuwa hatua itakayoonekana kama vile ni kuondowa vikosi lakini jambo hilo haliwezi kufanyika hivi karibuni.

Shambulio la jana ni baya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea tarehe 18 mwezi wa April ambapo watu 190 waliuwawa katika mashambulizi ya mabomu yaliotegwa kwenye magari katika maeneo ya Washia mjini Baghdad.

Leo miripuko ya mabomu kwenye magari imeuwa watu wanane katikati ya Baghdad.