1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baghdad. Kiongozi ataka raia wapewe silaha.

9 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBkV

Mmoja kati ya viongozi maarufu wa kisiasa nchini Iraq ametoa wito wa raia kupewa silaha.Hii ni baada ya mtu aliyejilipua kwa bomu kwa kujitoa muhanga kuuwa Wairaq 23 ambao walikuwa wamejiandikisha kuwa wanajeshi.Shambulio la bomu jana Jumapili katika mji wa Haswa kusini mwa Baghdad lilikuwa ni shambulio baya kabisa mwishoni mwa juma lililopita katika nchi hiyo ambayo imeathirika na vita. Mbunge wa chama cha Wakurd Mahmoud Othman amesema kuwa mpango wa usalama unaoendeshwa na Marekani hauwezi kufanya kazi, akisisitiza kuwa suala hilo linahusiana na wanasiasa na viongozi wa kidini nchini humo.

Wakati mapambano ya majeshi ya Marekani yakiendelea ndani na nje ya mji mkuu Baghdad wapiganaji wanashambulia maeneo ambayo hayana ulinzi wa kutosha, na makamu wa rais Tarek al – Hashemi ambaye ni msuni amesema kuwa Wairaq wanahaki ya kuwa na silaha ili kujilinda. Amesema kuwa serikali inapaswa kuwapa silaha , fedha na ujuzi kwa ajili ya hatua kama hizo za kiusalama lakini inapaswa kuweka udhibiti.