1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Maafa yazidi kuwakumba wamarekani Iraq.

31 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwF

Watu kiasi ishirini wameuawa na wengine kadha wamejeruhiwa baada ya shambulio la bomu kwenye kituo cha kusajili askari polisi wapya katika mji wa Fallujah, mkoa wa Anbaar.

Polisi wamesema mtu mmoja alijilipua kwa bomu alipokuwa akisubiri kwenye foleni pamoja na raia wengine waliotaka kuajiriwa kazi ya askari polisi.

Wakati huo huo majeshi ya Marekani nchini Iraq yamesema askari sita zaidi wa kimarekani wameuawa juma hili kwenye mashambulio katika maeneo mbali mbali nchini humo.

Kwa mujibu wa majeshi hayo, mwezi Mei ndio mwezi ambao wanajeshi wa Marekani wamewahi kupata maafa makubwa zaidi tangu mwaka 2004.

Askari wawili walifariki jana baada ya shambulio la bomu lililotegwa kando ya barabara karibu na mitaa hatari ya kusini mashariki mwa mji mkuu wa Baghdad.

Mauaji ya hivi karibuni yameongeza idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa kufikia askari elfu tatu mia nne na sabini na mmoja tangu vita vya Iraq vilipoanza mwezi machi mwaka 2003.

Takwimu hizo zimetokana na wizara ya ulinzi ya Marekani.