1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Marekani yailaumu Iran kwa kuwasaidia wapiganaji wa Irak

25 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBfS

Balozi wa Marekani nchini Irak, Ryan Crocker, amesema Iran imeongeza msaada kwa makundi ya wanamgambo nchini Irak katika miezi ya hivi karibuni.

Balozi Crocker amesema hayo baada ya kukutana na balozi wa Iran mjini Baghdad kwenye mazungumzo kuhusu usalama wa Irak baina ya Marekani na Iran ambayo ni nadra kufanyika.

Mazungumzo hayo yaliyoelezwa kuwa na ubishi, yalianza baada ya mwito kutolewa na waziri mkuu wa Irak kutaka msaada wa kujenga utengemano nchini humo.

Marekani inailaumu Iran kwa kuchochea machafuko nchini Irak huku Iran ikiitaka Marekani iondoe majeshi yake kutoka nchini humo. kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na gazeti la New York Times, nchini Marekani, majeshi ya Marekani yataendelea kubakia nchini Irak hadi msimu wa kiangazi mwaka wa 2009.

Gazeti hilo, likinukulu ripoti ya siri ya serikali ya Marekani, limesema mpango huo mpya umeandaliwa na balozi wa Marekani nchini Irak, Ryan Crocker, na kamanda wa jeshi la Marekani nchini humo, jenerali David Petraeus.