1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Marekani yajitoa lawamani kuhusu kunyongwa Saddam Hussein

3 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCde

Msemaji wa majeshi ya Marekani amesema vikosi vya nchi hiyo vilivyoko Iraq havikuhusika kwa vyovyote vile na kunyongwa Rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein, mara baada ya kumkabidhi kwa maafisa wa serikali ya Iraq.

Meja Jemedari William Caldwell amewaambia waandishi wa habari Marekani ingefuata utaratibu tofauti endapo ingetakiwa kutekeleza adhabu ya kifo dhidi ya Saddam Hussein.

Meja Jemedari William Caldwell ametoa tangazo hilo huku maandamano na upinzani mkali yakiendelea kutokana na jinsi adhabu ya Saddam Hussein ilivyotekelezwa.

Hapo awali serikali ya Iraq ilitangaza imeanzisha uchunguzi kuhusu ukanda wa video ulioonyesha jinsi alivyonyongwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Saddam Hussein.

Mshauri wa usalama wa Iraq, Muaffak el Rubbaie, alisema kifo cha Saddam kinapaswa kuuunganisha umma wa Iraq.

Muaffak alielezea kufadhaishwa na kitendo cha kunyongwa Saddam kunaswa kwenye ukanda wa video kwa kusema:

"Ninaamini aliingia mtu kwenye umati katika ukumbi huo. Watu hawa wamesababisha tatizo kubwa. Kwa hakika ninaamini huenda haya yalikuwa yamepangwa na kituo kimoja cha televisheni ya kiarabu"

Habari za hivi punde zinasema mmoja wa walinzi waliokuwa kwenye ukumbi alionyongewa Saddam Hussein amekamatwa kwa tuhuma za kupiga picha hizo.

Wakati huo huo vituo viwili vya televisheni vya Kiarabu vimearifu washtakiwa wawili waliopatikana na hatia pamoja na Saddam Hussein watanyongwa kesho.

Ndugu wa kambo wa Saddam, Barzan Ibrahim Al-Tikriti ambaye pia alikuwa mkuu wa upelelezi nchini Iraq na jaji mkuu wa zamani wa mahakama ya Iraq Awadh Ahmed Al-Bandar watanyongwa alfajiri ya kesho alhamisi.