1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Miripuko yatingisha Baghdad

25 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCOm

Kumekuwepo na repoti ya kutokea kwa miripuko kadhaa mikubwa ya mabomu mjini Baghdad waakati wa usiku.

Msemaji wa kijeshi amethibitisha kwamba wanajeshi wa Marekani wamefanya mashambulizi ya anga katika eneo hilo. Hakuna maafa yaliorepotiwa.

Pia katika mji mkuu huo wa Iraq waasi wamevamia kituo cha ukaguzi wa polisi karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad na kuuwa polisi wanane.Kadhalika gari la mafuta lililokuwa na mabomu limeripuka kwenye mji wa Habanniya ulioko kilomita 85 magharibi mwa Baghadad.Shambulio hilo ambalo limetokea mbele ya msikiti wa Wasunni limeuwa takriban watu 39 na kujeruhi nwengine 64.

Umwagaji damu huo umekuja wakati Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki akitowa tathmini nzuri juu ya msako wa usalama unaoendelea wa Marekani na Iraq katika mji mkuu wa Baghdad ambapo amesema wanamgambo 400 wameuwawa na kwamba mauaji ya kimadhehebu yamekuwa yakipunguwa.

Wakati huo huo Rais Jalal Talabani wa Iraq ameshutumu vikali wanajeshi wa Marekani kwa kumkamata mtoto wa kiume wa mojawapo wa viongozi mashuhuri kabisa wa Kishia nchini Iraq na ametakwa wahusika wachukuliwe hatua za kinidhamu.

Ammar Al Hakim mtoto wa mwanasiasa mashuhuri wa Kishia Abdul Aziz Al Hakim aliwekwa kizuizini pamoja na walinzi wake wa usalama wakati akiwa kwenye kivuko cha mpaka kati ya Iran na Iraq hapo Ijumaa.

Alishikiliwa kwa masaa kadhaa kabla ya kuachiliwa.