1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baghdad. Mkutano wa usalama wazikutanisha Mareikani na Iran.

11 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCKJ

Mkutano wa usalama uliofanyika jana Jumamosi mjini Baghdad chini ya uenyekiti wa serikali ya Iraq imepelekea kukutana kwa muda mfupi kati ya Iran na Marekani , kwa mujibu wa balozi wa Marekani Zalmay Khalilzad.

Amesema kuwa amewasilisha madai ya Marekani kuwa Iran inawapa silaha wapiganaji nchini Iraq.

Naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Abbas Araghchi, hata hivyo , amekana kuwa mazungumzo ya moja kwa moja yalifanyika.

Ameitaka Marekani kuondoa majeshi yake kutoka Iraq, akisema kuwa yanachochea hali ya machafuko.

Akihutubia mkutano huo uliohudhuriwa na mataifa 16, ikiwa ni pamoja na mataifa yenye kura ya veto katika umoja wa mataifa pamoja na jumuiya ya mataifa ya Kiarabu, waziri mkuu wa Iraq Nuri al-Maliki ameyataka mataifa hasimu katika eneo hilo kutounga mkono wapiganaji.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iraq Hoshiyar Zebari amesema kuwa mkutano huo ulikuwa wa mafanikio. Wakati maafisa wakikutana , mabomu mawili yalilipuka karibu na eneo la wizara ya mambo ya kigeni. Mashariki mwa Baghdad bomu lililokuwa katika lori limesababisha watu 26 kuuwawa katika kituo cha upekuzi kuelekea katika kitongoji cha Sadr City.