1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Wanajeshi tisa wa Marekani wauwawa

24 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC7a

Jeshi la Marekani nchini Irak limetangaza kwamba wanajeshi wake tisa wameuwawa na wengine 20 kujeruhiwa kwenye shambulio la bomu lililofanywa na mtu wa kujitoa mhanga maisha kaskazini mashariki mwa mji mkuu Baghdad.

Hujuma hiyo imetokea katika mkoa wa Diyala ambako wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakikabiliwa na mashambulio makali ya wapiganaji wa Irak.

Sambamba na taarifa hizo, wabunge wa chamna cha Democrats nchini Marekani wamepitisha mswada wa bajeti ya vita vya Irak na kuweka tarehe ya wanajeshi wa Marekani kuanza kuondoka nchini humo.

Wabunge hao wamechukua uamuzi huo licha ya kitisho kilichotolewa na rais George W Bush kutaka kuutilia guu mswada huo kutumia kura yake ya turufu. Kiasi ya dola bilioni 120 za Marekani zitatumiwa katika vita vya Irak lakini vikosi vya Marekani vinatakiwa kuanza kuondoka kuanzia Oktoba mosi mwaka huu.

Lengo lengine lisililo na mafungamano linataka wanajeshi wote wa Marekani wawe wameondoka Irak kufikia Aprili mosi mwaka ujao 2008.

Rais George W Bush amesema mara kwa mara atauzuia mswada wowote utakaoweka muda wa wanajeshi wa Marekani kuondoka kutoka Irak.