1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD : Watu 100 wauwawa Iraq

23 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYi

Nchini Iraq watu 100 wameuwawa katika mashambulizi mawili tafauti kwenye masoko mjini Baghdad na Baquba.

Watu 88 wameuwawa na wengine 160 kujeruhiwa katika mashambulizi mawili ya mabomu yaliotegwa kwenye magari katika soko la mitumba mjini Baghdad hilo likiwa ni shambulio baya kabisa kuwahi kushuhudiwa mwaka huu.Watu wengine 12 wameuwawa katika shambulio la bomu na mzinga katika mji jirani wa Baquba.

Mashambulizi hayo yanakuja wakati wanajeshi wa kwanza kati ya kikosi cha wanajeshi 21,000 wa ziada wa Marekani kilichoamuriwa na Rais George W. Bush kwenda Iraq wakiwa wamewasili mjini Baghdad kuimarisha hali ya usalama mjini humo.Wanajeshi wa Marekani wamekuwa wakipata kipigo kikubwa katika siku za hivi karibuni.

Hapo Jumamosi wanajeshi 25 wa Marekani wameuwawa katika mojawapo ya siku mbaya kabisa kwa jeshi la Marekani tokea ivamie Iraq.

Wakati huo huo naibu kiongozi wa kundi la Al Qaeda Ayman al Zawahri ameukejeli mpango wa Rais George W. Bush wa Marekani wa kutuma wanajeshi zaidi nchini Iraq kwa kusema kwamba wanamgambo wa mujahideen nchini Iraq wana uwezo wa kuliangamiza jeshi zima la Marekani.