1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Watu watatu wauawa mjini Kirkuk

16 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCIQ

Watu watatu wameuwawa leo na wengine wanane wakajeruhiwa kwenye mripuko wa bomu uliotokea mjini Kirkuk kaskazini mwa Irak.

Mripuko huo umefuatiwa na shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Irak ambapo maafisa wawili wa polisi na raia mmoja wameuwawa. Watu wengine wanane wakiwemo maafisa wanne wa polisi wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.

Polisi mjini humo wamepata maiti nne mbili ziikiwa za polisi waliokuwa na alama za mateso.

Haya yametokea kufuatia ripoti ya wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, inayosema mashambulio dhidi ya Wairaki na majeshi ya muungano yanayoongozwa na Marekani yamefikia kima cha juu zaidi katika kipindi cha zaidi ya miaka mitatu iliyopita.

Msemaji wa chama cha Democratic nchini Marekani, John Reid, haoni mafanikio yoyote ya mpango wa rais George W Bush nchini Irak.

´Nchi hiyo iko katika hali ya vurugu. Hakuna uthabiti nchini Irak. Vikosi vya jeshi la Marekani vinasimamia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Wairak na wala sio kuwasaka na kuwaua magaidi waliotushambulia mnamo tarehe 11 mwezi Septemba mwaka wa 2001.´

Wakati haya yakiarifiwa meya wa ngome ya Washia ya Sadr mjini Baghdad, Sheikh Raheem al Darruji ameponea chupuchupu jaribio la kutaka kumuua.

Kiongozi huyo amejeruhiwa wakati majambazi walipoifyatulia risasi gari yake. Afisa wa cheo cha juu katika jeshi la polisi ameuwawa katika shambulio hilo.

Meya huyo amekuwa akiwindwa kwa kupanga operesheni ya kuwasaka wapiganaji iliyofanywa na jeshi la Marekani na Irak katika eneo hilo.