1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD: Watuhumiwa wawili wakamatwa

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDU

Jeshi la Marekani nchini Irak limetangaza limewakamata watu wawili wanaotuhimiwa kuwa wanamgambo katika eneo la Sadr mashariki mwa mji mkuu Baghdad linalokaliwa na Washia.

Wanajeshi wa nchi kavu walikabiliwa na upinzani mkali wakati wa uvamizi wa eneo hilo lakini mashambulio ya adui yalizimwa na mashambulio ya angani yaliyofanywa na majeshi ya Marekani na Irak.

Duru zinasema nyumba moja imeharibiwa katika mashambulio hayo lakini hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa.

Wilaya ya Sadr ni ngome ya wanamgambo wa kishia na imekuwa kitovu cha uvamizi wa mara kwa mara tangu operesheni ya usalama ya jeshi la Marekani na Irak ilipoanza wiki saba zilizopita.

Wakati huo huo, watu waliokuwa na bunduki wamewashambulia kwa risasi wafanyakazi wa ujenzi waliokuwa ndani ya basi wakirejea nyumbani kutoka kazini katika kambi ya jeshi la Marekani yapata kilomita 290, kaskazini mwa Baghdad. Wafanyakazi tisa wameuwawa na mmoja kujeruhiwa katika hujuma hiyo.

Wizara ya mambo ya ndani ya Irak imetangaza kwamba Wairaki takriban 1,800 waliuwawa kwenye mashambulio ya mwezi uliopita.

Habari zaidi nchini Irak zinasema waziri wa sheria amejiuzulu kutoka kwa serikali inayoongozwa na waziri mkuu Nuri al Maliki.