1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baghdad.Idadi ya vifo vya wanajeshi wa Marekani vyaongezeka nchini Iraq.

30 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CCxn

Vifo vya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq katika mwezi huu wa October vimeongezeka na kufikia wanajeshi 100, baada ya mwanamaji wa Marekani kuuwawa hapo jana magharibi mwa jimbo la Anbar.

Jeshi la Marekani katika taarifa yake hii leo limesema mwanajeshi huyo alifariki katika mapigano, lakini halikutoa maelezo zaidi.

Kabla ya kifo cha mwanajeshi huyo, mwezi huu wa October ulikuwa tayari umeshajumuishwa kuwa ni mwezi unaoongoza kwa vifo tangu mwezi January mwaka 2005 ambapo wanajeshi wa Marekani 107 waliuwawa.

Idadi kuu zaidi ya vifo vya wanajeshi wa Marekani ilitokea mwezi November mwaka 2004 ambapo wanajeshi 137 waliuwawa na hivyo kuvunja rekodi ya vifo kwa wanajeshi hao walioko Iraq.

Idadi kamili ya wanajeshi waliouwawa tangu Marekani ilipoivamia Iraq mwezi March mwaka 2003 imefikia wanajeshi 2,813.

Hata hivyo wanajeshi wa Iraq waliouwawa ni wengi zaidi kuliko wanajeshi wa Marekani nchini humo, maana kamanda wa jeshi la Marekani nchini Iraq mnamo wiki hii amesema,polisi wa Iraq na wanajeshi 300 wameuwawa kufuatia kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani uliomalizika wiki chache zilizopita.

Wakati huo huo mamia ya raia huuwawa kila wiki kufuatia mashambulio ya kujitolea muhanga mna mashambulizi yanayofanywa na waasi.

Rais wa Marekani George W. Bush anakabiliwa na shinikizo kubwa kutokana na sera zake nchini Iraq, ikihofiwa chama chake cha Republican huenda kikapoteza viti katika uchaguzi wa baraza la Congress mwezi ujao.