1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAGHDAD:Mashambulio ya kujitoa muhanga yazidi kushuhudiwa Iraq

26 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCOS

Nchini Iraq mfululizo wa mashambulio ya mabomu umeshuhudiwa kote katika mji mkuu Baghdad hapo jana na kusababisha kuuwawa kwa watu zaidi ya 50.

Katika shambulio baya kabisa la kujitoa muhanga mshambuliaji alijiripua nje ya chuo na kuua watu kiasi 40 na kuwajeruhi wengine 35.

Kabla ya hapo makombora mawili yalivurumishwa katika eneo linalokaliwa na washia huko kusini mwa Baghdad na kuwauwa watu 12 na wanane wakajeruhiwa.

Watu wengine wawili waliuwawa na wengine wanane wakajeruhiwa katika shambulio jingine lililofanywa katika eneo lenye ulinzi mkali katikati mwa Baghdad.

Mashambulio hayo yametokea wakati waziri mkuu wa Iraq Nouri al Maliki akidai kwamba hatua imepigwa dhidi ya waasi mjini Baghdad na kwamba usalama umeimarishwa.Wakati huo huo kiongozi wanamgambo wakishia Moqtada al-Sadr amesema mpango wa usalama unaoungwa mkono na Marekani nchini Iraq hautafua dafu hadi pale serikali ya Iraq itakapochukua majukumu kamili ya kuwalinda raia wake.