1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya kimataifa yatoa hukumu mjini Arusha.

Abdu Said Mtullya18 Desemba 2008

Bagosora ahukumiwa kifungo cha maisha jela.

https://p.dw.com/p/GIah
Mabaki ya wahanga wa mauaji halaiki nchini Rwanda.Picha: AP


Mahakama ya Umoja wa Mataifa leo imetoa adhabu ya kifungo cha miasha jela kwa aliekuwa kanali wa jeshi la Rwanda Theoneste Bagosora baada kupatikana na hatia ya kushiriki katika mauaji ya watu 800,000 nchini Rwanda mnamo mwaka 1994.

Mahakama maalumu ya kimataifa,ICTR ya mjini Arusha, Tanzania inayoshungulikia mauaji halaiki yaliyofanyika nchini Rwanda, ilimfungulia mashtaka Bagosora ya kuwa kiongozi wa vikosi vya jeshi na wa wanamgambo wa kihutu Interahamwe, waliowaangamiza watusi pamoja na wahutu waliokuwa na mtazamo wa ukadirifu.

Mahakama hiyo ilimtia hatiani Bagosora kwa kushiriki katika mauaji ya kimbari ,uhalifu dhidi ya ubinadamu na kwa kutenda uhalifu wa kivita.

Katika tamko la kumtia hatiani , Bagosora mwenye umri wa miaka 67, mahakama ya kimataifa ilisema kuwa kabla ya mauaji,Bagasora alisusia mazungumzo ya amani nchini Tanzania na kusema anarejea nyumbani " kutayarisha kihama".

Bagosora alikuwa mkurugenzi katika wizara ya ulinzi ya Rwanda wakati ndege ya aliekuwa rais wa nchi hiyo, Juvenal Habyarimana ilipotunguliwa.Kifo cha rais huyo ndicho kilichosababisha mauaji halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Mtu mwengine aliehukumiwa leo na mahakama ya kimataifa mjini Arsuha ni Protais Zigiranyirazo. Mfanyabiashara huyo ambae ni shemeji wa hayati Habyarimana amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuwa mwanachama wa kundi la Akazu la watu waliokula njama za kuwaangamiza watusi.