1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BAIDOA:bunge lateua spika mpya Somalia

1 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCWG

Wabunge nchini Somalia wamemteua mbabe wa kivita wa zamani kuwa Spika mpya wa Bunge baada ya kumtimua spika wa zamani aliyekutana kinyume na sheria na wawakilishi wa mahakama za kiislamu .

Wabunge hao walimuidhinisha Waziri wa Sheria Aden Mohammed Nur kuwa Spika wa Bunge bila pingamizi ,siku moja baada ya Rais Abdullahi Yusuf kujaribu kutafuta kuungwa mkono katika serikali yake inayozongwa na matatizo.Sharif Sheik Aden alitimuliwa katikati ya mwezi jana.

Wabunge 153 kati ya wote 112 waliohudhuria kikao cha bunge waliidhinisha uteuzi huo.

Aden Mohammed Nur aliye mwandani wa karibu wa Rais Yusuf alikuwa mwalimu wa Koran tukufu aliyebadilika kuwa mbabe wa kivita.Kiongozi huyo anatoka ukoo wa Digil-Mirifle ulio na wakazi wengi katika eneo la kusini mwa kusini mwa Somalia.

Uteuzi huo unatokea siku moja baada ya Rais Yusuf kutoa wito wa ushirikiano na maridhianao ya kitaifa ili kuungwa mkono katika serikali inayozongwa na mivutano.

Kutimuliwa kwa Sheik Aden kulizua tetesi katika jamii ya kimataifa iliyo onya kuwa hatua hiyo huenda ikachochea ghasia kati ya koo zinazowakilishwa serikalini.

Bwana Nur ana jukumu la kuongoza Bunge la wanachama 275 lililoundwa katika nchi jirani ya Kenya mwaka 2004 baada ya miaka miwili ya majadiliano.

Bunge la Somalia linawakilisha koo nne kubwa nchini humo za Darood,Digil-Mirifle,Dir na Hawiye.Kila ukoo una wawakilishi 61 huku koo ndogo zilizosalia zina nafasi 31.