1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ban ambana Machar kurejea haraka Juba

23 Aprili 2016

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon Ijumaa (22.04.2016) amemuwekea mbinyo zaidi kiongozi wa waasi nchini Sudan kusini Riek Machar kurejea mjini Juba "bila kuchelewa" na kuanza kazi katika serikali ya mpito.

https://p.dw.com/p/1IbEo
Südsudan Rebellenführer Riek Machar
Kiongozi wa waasi Sudan kusini Riek MacharPicha: Reuters/G. Tomasevic

Machar alitarajiwa kurejea katika mji mkuu siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa yenye lengo la kumaliza vita vya miaka miwili, lakini tofauti kuhusiana na mipango ya kiusalama mjini Juba inachelewesha kurejea kwake.

Ban amesema serikali ya rais Salva Kiir imekubali pendekezo la muafaka kuhusiana na matayarisho ya kurejea kwa Machar na kusema hatua hii inapaswa kusaidia kuundwa kwa haraka kwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa.

Südsudan Rebellenführer Riek Machar
Makamu wa rais mtarajiwa Riek Machar wa Sudan kusiniPicha: Reuters/T. Negeri

"Kuendelea na hali ya ushirikiano itakuwa muhimu wakati viongozi wa nchi hiyo wakianza mchakato wa kubadilisha miaka ya uharibifu uliosababishwa na mzozo huo kwa watu wa Sudan kusini," amesema katika taarifa.

Mateso ya watu wa Sudan kusini

Ban amemtaka Machar kusafiri kwenda Juba " bila masharti zaidi" hali ambayo inaweza kuchafua mchakato wa amani na kuendeleza hali ya mateso yanayowakuta watu wa Sudan kusini."

Chini ya makubaliano ya amani, Machar alitakiwa kurejea tena katrika wadhifa wake wa makamu wa rais katika serikali mpya itakayodumu kwa muda wa miezi 30 na kuielekeza nchi hiyo katika uchaguzi mkuu.

Schweiz UN Ban Ki-moon in Genf
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moonPicha: Reuters/D. Balibouse

Kikwazo cha hivi sasa kinahusiana na idadi ya bunduki na vifaa vya kufyatulia maguruneti ambavyo vikosi vya waasi vinavyomlinda Machar vitaruhusiwa kuwa navyo.

Vita vya Sudan kusini vilianza Desemba mwaka 2013, wakati Kiir alipomshutumu Machar kwa kula njama za kumpindua. Mzozo huo umeweka wazi mpasuko wa tofauti za kikabila na umekuwa ukionesha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na ubakaji wa makundi, uchomaji moto vijiji na hata ulaji nyama za watu.

Ombi la Marekani

Kwa ombi la Marekani, baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikutana siku ya Jumatatu na kuelezea "wasi wasi wake mkubwa " kwa kushindfwa kurejea Machar mjini Juba.

Südsudan-Verhandlungen vorerst gescheitert
Rais wa Sudan kusini Salva Kiir (kulia)Picha: Reuters/Jok Solomun

Jumuiya zenye nguvu duniani, ikiwa ni pamoja na Umoja Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya , China , Uingereza na Marekani , zimewapatia Machar na Kiir muda wa mwisho hadi leo Jumamosi (23.04.2016) kutatua tofauti zao.

Mamia kwa maelfu ya watu wameuwawa na zaidi ya watu wengine milioni mbili wamelazimika kuyakimbia makaazi yao tangu vita hivyo vilipozuka Desemba mwaka 2013.

Wasiwasi unatuwama katika hali ya kutoaminiana kuhusiana na silaha hali ambayo imechelewesha kurejea kwa Machar.

Sudan Darfur Konflikt Soldaten
Wanajeshi wa jeshi la serikali ya Sudan kusiniPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Kikosi cha wanajeshi waasi wapatao 1,370 tayari kimewasili mjini Juba kama sehemu ya makubaliano ya amani wakati majeshi ya serikali yanasema yameondoa wanajeshi wake wote isipokuwa wanajeshi 3,420 , kwa mujibu wa makubaliano. Wanajeshi wengine wote wanapaswa kubakia kiasi ya kilometa 25 nje ya mji mkuu.

Katika moja kati ya kambi tatu za waasi mjini Juba, waasi wanatengana na kambi ya majeshi ya serikali kiasi ya mwendo wa miguu wa dakika tano na wanaweza kuonana na karibu iwapo kutatokea rabsha zozote.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afp

Mhariri: Bruce Amani