1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bangladesh yatenganisha Mahakama na Serikali

P.Martin5 Novemba 2007

Mahakama za Bangladesh zimefanikiwa kukata minyororo ya ushawishi wa serikali na urasimu. Sasa kinachongojewa ni kuona vipi mabadiliko hayo makubwa yatasaidia kutekeleza sheria halisi kwa umma.

https://p.dw.com/p/C7fV

Juma lililopita,katika sherehe ya kihistoria mjini Dhaka,kiongozi wa serikali ya mpito ya Bangladesh,Fakhruddin Ahmed na Jaji Mkuu Ruhul Amin walitangaza rasmi hatua ya kutenganisha mahakama na serikali.Sasa ni Mahakama Kuu na si serikali inayowajibika kuteua majaji na mahakimu.Akieleza mabadiliko hayo Amin alisema,wanasheria sasa watadhibiti mamlaka,lakini hayo kwa kweli si mamlaka bali ni ahadi ya kufuta machozi yaliyosababishwa na dhulma.

Miaka minane iliyopita,Mahakama Kuu iliiomba serikali kuchukua hatua ya kutenganisha mahakama na serikali.Lakini serikali za mawaziri wakuu wote wawili wa zamani,yaani Sheikh Hasina Wajed na Khaled Zia ambao hivi sasa wapo jela-hawakufanya mageuzi hayo walipokuwa madarakani. Si vyama wala wanasiasa waliotaka kweli,kutoa uhuru kwa mahakama zilizopoteza imani ya umma kwa sababu ya shinikizo za kisiasa na serikali kuingilia kati.

Kwa hivyo,jukumu hilo limeiangukia serikali ya mpito inayoongozwa na mchumi Fakhruddin Ahmed, ambae hapo zamani alifanya kazi katika Benki ya Dunia.Ahmed alinyakua madaraka kwa msaada wa jeshi kufuatia mapambano ya umwagaji damu mitaani kati ya wafuasi wa mahasimu wawili wakuu wa kisiasa.Mapambano hayo yalihusika na utaratibu wa uchaguzi mkuu uliotazamiwa kufanywa Januari mwaka huu.

Uamuzi wa kutenganisha mahakama na serikali umepingwa na baadhi kubwa ya wanasiasa.Mwishoni mwa mwezi wa Oktoba,zaidi ya maafisa 600 serikalini,waliandamana mji mkuu Dhaka katika juhudi ya kushawishi uamuzi utakaowanyanganya mamlaka ya mahakama yaliyokuwa mikononi mwa serikali tangu enzi ya ukoloni wa Uingereza.

Hali ya hatari imetangazwa nchini Bangladesh, tangu serikali ya mpito kushika madaraka.Rais Ahmed anaetaka kuitisha uchaguzi ulio huru na wa haki mwishoni mwa mwaka ujao,amesema kwanza atapiga vita rushwa na atafanya mageuzi kadhaa yalio na dharura.

Kwa mujibu wa mwanasheria mashuhuri Kamal Hossain,katiba ya Bangladesh iliyoandikwa mwaka 1972,imeeleza wazi wazi kuwa mahakama zinapaswa kutenganishwa na serikali.Hossain aliesaidia kutayarisha katiba hiyo na kufanya kazi kama waziri wa nje katika serikali ya muasisi wa Bangladesh-marehemu rais Sheikh Mujibur Rahman, amesema madai ya kutenganisha mahakama na serikali yalianza tangu Bangladesh kupata uhuru wake kutoka Pakistan.

Lakini utaratibu huo haukuweza kutekelezwa hapo mwanzoni kwa sababu ya uhaba wa wafanyakazi, kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe kugombea uhuru kutoka Pakistan.Na Sheikh Mujibur Rahman alipouawa katika mwaka 1975,utaratibu huo ulisitishwa.Sasa hatua ya kwanza ya kuwa na mahakama huru imechukuliwa na hivyo madai ya umma ya muda mrefu yametekelezwa.