1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa lapitisha azimio dhidi ya Syria

Josephat Nyiro Charo17 Februari 2012

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio linalotaka ukandamizaji nchini Syria ukome mara moja. Azimio linamtaka rais wa Syria, Bashar al Assad aondoke madarakani.

https://p.dw.com/p/144eI
Members of the United Nations General Assembly vote to endorse the Arab League's plan for Syria's President Bashar al-Assad to step aside, at the United Nations Headquarters in New York February 16, 2012. The 193-nation U.N. General Assembly on Thursday overwhelmingly approved a non-binding resolution endorsing an Arab League plan that urges Syrian President Bashar al-Assad to step aside. REUTERS/Andrew Kelly (UNITED STATES - Tags: POLITICS)
UN Vollversammlung stimmt zur Syrien Resolution abPicha: Reuters

Kwenye azimio lenye maneno makali ambalo lilipigiwa kura 137 kwa 12, mataifa wanachama ya Umoja wa Mataifa yameutaka utawala wa rais Assad ukomeshe ukandamizaji dhidi ya waandamanaji na uanze kuwaondoa wanajeshi kutoka mijini na kuwarudisha kambini.

China, Urusi na Iran zililipinga azimio hilo lililoandaliwa na nchi za kiarabu zikiungwa mkono na nchi za magharibi, siku chache tu baada ya China na Urusi kulipinga azimio kama hilo katika baraza la usalama la umoja wa Mataifa. Hatua ya baraza kuu inaongeza shinikizo dhidi ya rais Assad kukomesha ukandamizaji ambao umesababisha watu 41 kuuwawa hapo jana wakati vikosi vya usalama vilipoyashambulia maeneo ya wapinzani wa serikali.

Balozi wa Misri katika Umoja wa Mataifa, Osama Abdelkhalek, amesema baraza kuu la umoja huo limetuma ujumbe wa wazi kwa utawala wa mjini Damascus kuwa wakati umewadia kusikiliza kilio cha wananchi.

Lakini mjumbe wa Syria katika umoja huo, Bashar Jaafari, kwa upande wake amelikataa azimio hilo akilieleza kuwa njama ya kuipindua serikali ya rais Assad na kuuruhusu upinzani kuichukua nchi. Ameyakosoa mataifa ya kiarabu akisema nchi za magharibi zimeutumia vibaya umoja wa nchi za kiarabu kuufanya mzozo wa Syria kuwa wa kimataifa.

Syria's Ambassador to the United Nations (U.N.) Bashar Jaafari (C) speaks with China's Ambassador Li Baodong (L) as they arrive at the U.N. Security Council to discuss a European-Arab draft resolution endorsing an Arab League plan calling for Syria's President Bashar al-Assad to give up power in New York February 4, 2012. The Homs attack made Friday the bloodiest day of an 11-month uprising and it gave new urgency to a push by the Arab League, the United States and Europe for a U.N. resolution calling for Assad to cede power. The Security Council had scheduled an open meeting for Saturday to vote on the draft. But Russia asked that the 15-nation body not immediately do so and instead hold consultations. REUTERS/Allison Joyce (UNITED STATES - Tags: POLITICS)
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bashar Jaafari (katikati)Picha: Reuters

Naye balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Mohammad Khazaee, ameonya kwamba azimio hilo litauzidisha mzozo ndani ya Syria na kuongeza athari katika eneo zima kwa ujumla.

Balozi wa Ujerumani katika Umoja wa Mataifa, Peter Witig, amelipongeza azimio hilo akisema linadhihirisha kuwa jamii ya kimataifa haitawasahau wananchi wa Syria.

"Hii ni ishara nzito kwa jumuiya ya kimataifa, lakini hasa kwa utawala wa Syria kwamba sasa unalazimika kukomesha machafuko. Ni ishara nzito pia ya kuunga mkono umoja wa nchi za kiarabu na ujumbe huu unatoka moja kwa moja kutoka New York."

Urusi haikufurahishwa na hatua ya baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Balozi wa nchi hiyo katika umoja huo, Vitaly Churkin, amesema azimio hilo linaonyesha mkondo wa kutia wasiwasi kujaribu kuutenga utawala wa Syria, kukataa mawasiliano yoyote nao na kushinikiza mbinu kutoka nje kufikia suluhu ya kisiasa.

Nchini Syria kwenyewe wanajeshi wameushambulia mji wa Homs leo. Kwa mujibu wa mwanaharakati mmoja aliyeko mjini humo, maroketi manne yamevurumishwa kwa kila dakika moja katika vitongoji vya Khaldiyeh na Bayyada, kwenye operesheni inayoelezwa kuwa kali kabisa kuwahi kufanywa na vikosi vya Syria.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Hamidou, Oumilkheir