1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Mawaziri la Misri lakutana kujadili machafuko

10 Oktoba 2011

Serikali ya Misri imeitisha kikao cha dharura cha Baraza la Mawaziri hivi leo, baada ya makabiliano makali kati ya wanajeshi na Wakristo wa madhehebu ya Coptic yaliyosababisha mauaji na majeruhi kadhaa.

https://p.dw.com/p/12ojF
Mfuasi wa madhehebu ya Coptic akiinua msalaba mjini Cairo.
Mfuasi wa madhehebu ya Coptic akiinua msalaba mjini Cairo.Picha: dapd

Watu 23 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika vurugu zilizozuka baada ya waumini wa madhehebu ya Coptic kuandamana wakilalamikia mashambulizi ya karibuni dhidi ya kanisa lao.

Waandamanaji waliwashambulia wanajeshi kwa mawe na chupa nje ya jengo la televisheni ya taifa mjini Cairo, huku vurugu zikienea hadi uwanja wa Tahrir. Inaripotiwa kuwa baadhi ya waandamanaji waliwapokonya wanajeshi silaha na kuwageukia nazo. Waandamanaji wenyewe wanasema kuwa maandamano yao yalianza kwa amani, lakini baadaye wakashambuliwa na kundi la wahuni.

Wakristo nchini Misri wanaulaumu utawala wa kijeshi kwa kutokuchukuwa hatua zinazofaa dhidi ya wimbi la mashambulizi dhidi yao tangu kuangushwa kwa Hosni Mubarak hapo Februari.

Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR
Mhariri: Thelma Mwadzaya