1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Mpito la Libya lachagua waziri mkuu mpya

1 Novemba 2011

Wajumbe wa Baraza la Mpito nchini Libya jana wamemteuwa msomi na mfanyabiashara atakayeongoza serikali ya mpito ya nchi hiyo wakati huu Jumuiya ya Kujihami ya NATO ikiwa imehitimisha operesheni yake.

https://p.dw.com/p/132hm
Waziri Mkuu mpya wa Libya Abdel-Rahim al-KeibPicha: picture-alliance/dpa

Abdel Rahim al-Keib, mzaliwa wa Tripoli amechaguliwa kuwa waziri mkuu katika mchakato wa upigaji kura wa wazi uliofanywa na wanachama wa Baraza la Mpito la waasi.

Keib, ambaye hajulikani sana mpaka sasa, na msomi aliyejikita katika taaluma ya uhandisi umeme aliwashinda washiriki wengine wanne kwa kuongoza kwa kura 26 kati ya 51.

Akizungumza muda mfupi baada ya kukamilika kwa zoezi hilo, kiongozi wa Baraza la Mpito la nchi hiyo, Mustafa Abdel Jalil alisema zoezi hilo linathibitisha kwamba Walibya wapo tayari kujenga nchi yao.

Abdul al-Rahim al-Kib Chef Übergangsrat in Libyen
Keib akipongozwa baada ya ushindiPicha: picture-alliance/dpa

Keib ana sifa zote kielimu na mfanyabiashara aliyefanikiwa ambaye ameishi miongo kadhaa nje ya nchi hiyo kama mpinzani wa Muammar Gaddafi, kabla hajajiunga na upande wa waasi ambao ulimuondoa madarakani kiongozi huyo wa zamani.

Waziri Mkuu huyo mpya wa serikali ya mpito pia ametajwa kuwa ni mtu aliyekuwa akilisadia baraza la mpito kifedha.

Akimwelezea Keib, Waziri wa Mambo ya ndani wa NTC, amesema shabaha yake kubwa ya kiongozi huyo mpya ilikuwa kustawisha hali ya usalama nchini humo na kusema uwepo wake utafanikisha hilo pamoja na jeshi kuwa katika udhibiti.

Lakini pia Waziri Mkuu Mpya wa NTC ameahidi kufanikisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa Walibya. "Nina imani kubwa na watu wa Libya, nina imani kubwa na wenzangu katika baraza la mpito la Libya, lakini pia ina imani ya mafanikio kwa kuishi katika nchi yenye rasilimali ya kutosha" alisema Keib.

Hapo awali Katibu Mkuu wa NATO, Anders Fogh Rasmussen ambaye aliwasili nchini humo alizungumza kidogo kwa kusema haoni kama kuna jukumu lolote kubwa kwa jumuiya hiyo lililosalia.

Wakati wa usiku, akizungumza katika mkutano wake pamoja na Mustafa Abdel Jalil mbele ya waandishi wa habari, Rasmussen alisema ukurasa wa mafanikio wa NATO imefikia kikomo."Kuanzia sasa ni jukumu la Baraza la Mpito la Libya kusimamia jukumu la ulinzi, lakini baraza hilo lina uhuru wa kuomba msaada wa kutoka kwa nchi tofauti" alisema Rassmussen.

Kuwasili kwa Katibu Mkuu huyo wa NATO kunafanyika baada ya miezi saba ya operesheni ya umoja huo ilishiriki nafasi kubwa katika kumuondoa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.

Operesheni ya kuzuia ndege kuruka kwa lengo la kuwalinda raia wa Libya iliongozwa na NATO kuanzia Machi 31 na kumalizika rasmi jana na hivyo kufikisha mwisho wa utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Sudi Mnette//AFP
Mhariri:Josephat Charo