1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Senet lapinga mswaada wa sheria kuondowa marufuku ya mashoga jeshini

Oumilkher Hamidou22 Septemba 2010

Serikali ya rais Barack Obama yashindwa kulazimisha katika baraza la Senet marufuku waliyowekewa mashoga jeshini yabatilishwe

https://p.dw.com/p/PJWU
Waziri wa ulinzi wa Marekani Robert Gates ni miongoni mwa wanaounga mkono marufuku hayo yabatilishwePicha: AP

Baraza la Senate nchini Marekani limezuwiya jaribio la kuondowa marufuku kwa mashoga kutumika jeshini bila ya kificho na hiyo kuzima hatua ya mbinu za kisiasa kwa kuliweka kando suala hilo kwa muda usiojulikana. .

__________________

Wafuasi wa chama cha Demokratik wanaotaka kutenguliwa kwa sera ya 'Usiulize,Usiseme' muafaka uliofikiwa mwaka 1993 kwa lengo la kutatua suala hilo gumu walikumbana na kizingiti cha upinzani wa chama cha Republican hapo jana.

Jumla ya maseneta 56 dhidi ya 43 walipiga kura kuendeleza mbele mjadala huo wakati wa kujadili matumizi ya kila ya mwaka ya wizara ya ulinzi ya Marekani ambapo kwayo kumeambatanishwa pendekezo hilo la kutenguliwa kwa marufuku hiyo kwa mashoga. Kulikuwa na upungufu wa kura nne katika kura 60 zinazohitajika kulipeleka mbele suala hilo.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs amesema wamekatishwa tamaa kwa kushindwa kulifanya pendekezo hilo kuwa sheria lakini wataendelea kujaribu. Kauli yake hiyo inakuja baada ya maseneta wa Demokrat Mark Pryer na Blanche Lincoln pia kupiga kura dhidi ya pendekezo hilo.

Katika kipindi kisichozidi miezi miwili kabla ya uchaguzi mdogo wa mwezi Novemba nchini Marekani uchunguzi wa maoni unaonyesha umma wa Marekani unaunga mkono kwa wingi kukomeshwa kwa sera hiyo inayowataka wanajeshi kuficha ushoga wao au venginevyo kutimuliwa jeshini.

Wanaokosoa sera hiyo wanadai kwamba marufuku hiyo inakiuka haki za kiraia za wanajeshi mashoga na imeleta madhara kwa usalama wa taifa wa Marekani kwani wanajeshi wenye ujuzi 14,000 wametimuliwa jeshini.

Makundi ya kutetea haki za mashoga ambayo yalifanya kampeni kali ya kutaka kuondolewa kwa sera hiyo yamevunjwa moyo na matokeo hayo.Rea Carey mkurugenzi mtendaji wa Kikosi- Kazi cha Taifa cha Mashoga na Wasagaji amesema maseneta waliongoza na kuunga mkono mbinu hiyo ya kukwamisha suala hilo wanapaswa kuona aibu .Ameita kura hiyo kuwa ni ya kukatisha tamaa na kutolitakia mema taifa.

Lakini Generali mwandamizi James Amos ameiambia Kamati ya Huduma za Jeshi katika baraza la Senate kwa ushahidi wa maandishi kwamba wanajeshi wa Marekani kwa kiasi kikubwa sana wanapinga kuondolewa kwa marufuku hiyo.

Amos ambaye anawekewa matumaini ya kuwa mkuu wa majeshi ya Marekani pia amesema kwamba anapinga kubadili sheria juu ya suala hilo ambayo anaielezea kuwa ni muafaka mzuri.

Katika ushahidi huo Amos ameandika kwamba pia ana wasi wasi kufanya mabadiliko wakati huu kunaweza kuwababaisha wanajeshi wa Marekani walioelekeza juhudi zao katika operesheni za mapambano nchini Afghanistan.

Wizara ya ulinzi wa Marekani inafanya tathmini ya mwaka mzima juu ya kutengua sera hiyo na tathmini yake inatarajiwa kukamilika kabla ya kumalizika mwezi wa Desemba jambo ambalo litasaidia kutunga sheria mpya juu ya huduma za jeshi.

Waziri wa Ulinzi Robert Gates halikadhalika Adimeri Mike Mullen ambaye ni mwenyekiti wa jopo la Wanadhimu Wakuu wa Majeshi wameunga mkono kuondolewa kwa marufuku hiyo.

Mwandishi:Mohamed Dahman/AFP

Mpitiaji: Josephat Charo