1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Marekani yaidhinisha msaada kwa Ukraine

24 Aprili 2024

Baraza la Seneti la Marekani limeidhinisha Jumanne usiku, kifurushi cha msaada wa mabilioni ya dola kwa Ukraine, Israel na Taiwan.

https://p.dw.com/p/4f74v
Marekani | Jengo la Capitol mjini Washington
Kifurushi cha msada huo kilipitishwa kwa kura nyingi katika Baraza la SenetiPicha: picture-alliance/dpa/Bildfunk/epa/J. L. Scalzo

Rais Joe Biden ndiye anayetakiwa kukamilisha mchakato huo kwa kutia saini na ameapa kuwa vifaa zaidi vitawasilishwa haraka kwenye eneo la vita huko Ukraine.

Tayari Rais wa Ukraine  Volodymyr Zelensky ameipongeza hatua hiyo  ya Baraza la Seneti kuidhinisha karibu dola bilioni 61 kwa taifa hilo ili kuisaidia kukabiliana na uvamizi wa Urusi. Kumeidhinishwa pia fedha za msaada wa kibinaadamu unaohitajika kwa Gaza, Sudan na Haiti.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Gints Ivuskans/AFP

Katika jumla ya msaada huo wa dola bilioni 95, kiasi dola bilioni 61 zimetengwa kwa ajili ya jeshi la Ukraine ambalo linahitaji mno silaha na wanajeshi wapya.

Soma pia: Ukraine yasifu Bunge la Marekani kuidhinisha msaada wa kijeshi

Muswada huo unaotarajiwa kuwa sheria umeafiki kutoa pia dola bilioni 26 za msaada kutokana na vita vya Israel na dola bilioni 8 ili kukabiliana na ushawishi unaoongezeka wa China huko Taiwan na katika kanda ya Indo-Pacific.

Muswada huo umejumuisha pia uwezekano wa kuupiga marufuku mtandao wa kijamii wa TikTok nchini Marekani, ikiwa wamiliki wa China hawatouza hisa zao ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

(Vyanzo: DPAE, AFPE)