1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Seneti lapitisha muswada wa "mkwamo wa bajeti "

1 Januari 2013

Ikulu ya Marekani na wabunge waandamizi wa chama cha Republikan wafikia makubaliano kuepusha ongezeko kubwa la kodi la Mwaka Mpya na kuahirisha kubana matumizi mambo yaliokuwa yakitishia kuuzorotesha uchumi wa Marekani.

https://p.dw.com/p/17C2L
Bunge la Marekani.
Bunge la Marekani.Picha: Getty Images

Baada ya miezi mingi ya usumbufu juu ya mzozo huo, wiki kadhaa za mjadala kuhusu ufumbuzi unaoweza kufikiwa na siku kadhaa za mazungumzo mazito ya faragha,wabunge wa Marekani wa baraza la Seneti walipiga kura kwa sauti kubwa 88 za kuunga mkono na nane za kupinga kuupitisha muswada huo tata mapema Jumanne(01.01.2013) ambao umeepusha kile kinachojulikana kama "mkwamo wa bajeti.".Muswada huo sasa unafikishwa katika Baraza la Wawakilishi la bunge la Marekani ambapo wataupigia kura baadae Jumanne katika Siku ya Mwaka Mpya.Rais Barack Obama katika taarifa amelihimiza baraza hilo kuuidhinisha muswada huo bila ya kuchelewa.

Iwapo muswada huo utakuwa umekubaliwa na mabaraza yote mawili ya bunge la Marekani kutampa ushindi Rais Obama kwa kuongeza viwango vya kodi kwa familia zenye kujipatia mapato yanayopindukia dola 450,000 kwa mwaka na ambapo hakuna mtu mwengine yoyote yule atakayejumuishwa kwenye mpango huo wa ongezeko la kodi.Obama amesema katika taarifa wakati sio chama cha Demokrat wala Republican waliopata kila kile waliochokuwa wanataka, makubaliano hayo ni kitu sahihi kwa nchi yao na kwamba Baraza la Wawakilishi linapaswa kuyapitisha bila ya kuchelewa.Makubaliano hayo yanaahirisha mpango wa kupunguza matumizi ya bajeti ya dola bilioni 109 kwa serikali kwa kipindi cha miezi miwili lakini mchakato huo unaanzisha mpambano mpya kati ya wabunge wa chama cha Demokrat na wa Republican mwishoni mwa mwezi wa Februari.Obama amesema "kuna kazi nyingi za kufanya kupunguza nakisi zetu,na niko tayari kufanya hivyo."

Rais Barack Obama akizungumzia uwezekano mkubwa wa kufikiwa makubaliano hayo 31.12.2012.
Rais Barack Obama akizungumzia uwezekano mkubwa wa kufikiwa makubaliano hayo 31.12.2012.Picha: Reuters

Biden alikuwako bungeni kushinikiza makubaliano

Makamo wa Rais Joe Biden ambaye ndie aliesaidia kufanikisha kufikiwa makubaliano hayo na mbunge mwandamizi wa Seneti wa chama cha Republikan Mitch McConnell amefika makao makuu ya bunge la Marekani kuunadi mpango huo kwa maseneta wa chama cha Demokrat ambao baadhi yao walikuwa wakitaka ongezeko hilo la kodi lianze kwa kiwango cha chini.Ingelikuwa makubaliano hayo hayakufikiwa wataalamu walionya kwamba uchumi dhaifu wa Marekani ungelianza tena kuzorota kutokana na mgao uliochanganywa wa dola bilioni 500 wa ongezeko la kodi na ubanaji wa matumizi ya serikali.Makubaliano hayo yalifikiwa masaa machache kabla ya muda wa mwisho wa usiku wa manane .Kura hiyo ya baraza la Seneti ilipigwa saa nane usiku saa za Marekani.

Makamo wa Rais Joe Biden akiwa bungeni kushinikiza makubaliano.
Makamo wa Rais Joe Biden akiwa bungeni kushinikiza makubaliano.Picha: Getty Images

Kazi iko kwa Baraza la Wawakilishi

Suala hilo sasa liko kwenye mikono ya Spika wa Baraza la Wawakilishi John Boehner kuunganisha wabunge kuunga mkono makubaliano hayo jambo ambalo yumkini likahitaji kura za chama cha Demokrat ili kuweza kupitishwa.Kwa miongo miwili wabunge wa chama cha Republikan walipinga jaribio lolote lile la kuongeza kodi kwa hiyo maafisa wa Ikulu ya Marekani wataona kuwa ni uthibitisho ulioko katika makubaliano hayo kuenzi mojawapo ya ahadi kuu za Obama alizotowa wakati wa kampeni zake za kuwania kuchaguliwa tena kuwa rais wa Marekani.Bohner amesema baraza lake litapitisha muswada huo baada ya kuidhinishwa na baraza la Seneti.

John Boehner Spika wa Baraza la Wawakilishi wa chama cha Repuplikan.
John Boehner Spika wa Baraza la Wawakilishi wa chama cha Repuplikan.Picha: Getty Images

Makubaliano yanafaa

Wabunge wa chama cha Demokrat wamedokeza kwamba kama vile ilivyo kwa makubaliano mengine yanayofikiwa bungeni sio kwamba ni kamilifu lakini yanafaa kuliko kuwa na mbadala wa huo.Seneta Chuck Schumer amewaambia waandishi wa habari kwamba sio kwamba pendekezo hilo ni adhimu au kwamba linapendwa kwa njia yoyote ile,lakini ni bora zaidi kuliko kuingia kwenye mkwamo wa bajeti.Obama awali alikuwa akitaka ongezeko la kodi lianzie kwa familia zenye mapato ya dola 250,000.Rais huyo amesema makubaliano hayo yataendelea kutowa mikopo ya kodi kwa kampuni za nishati safi isiochafuwa mazingira na pia kwa bima za ukosefu wa ajira kwa ajili ya watu milioni mbili ambazo muda wake ulikuwa umalizike.Makubaliano hayo pia yanajumuisha kumaliza upunguzaji wa muda wa asilimia mbili kwa kodi za Usalama wa Jamii kwa ajili ya akiba ya uzeeni na mabadiliko katika kodi za urithi na uwekezaji.

Mwandishi :Mohamed Dahman/AFP

Mhariri : Ssessanga Iddi