1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama lajadili hatima ya mashoga

Admin.WagnerD25 Agosti 2015

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana limejadili ukatili unaofanywa na kundi la Dola la Kiisalamu IS dhidi ya mashoga nchini Syria na Iraq, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa baraza hilo wa kutetea haki za mashoga.

https://p.dw.com/p/1GL6o
UN Abstimmung Iran Atomabkommen
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: Reuters/M. Segar

Katika mkutano huo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliozungumzia ukatili na ubaguzi dhidi ya mashoga, wasagaji pamoja na watu wanaozaliwa wakiwa na jinsia mbili, mkuu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za mashoga amesema, kundi la IS limekubali kuhusika na kuuwa takriban watu 30 kwa kujihusisha na matende ya ulawiti.

"Tunataka suala hili litambuliwe na Umoja wa Mataifa, lakini mpaka hii leo Baraza la Usalama halikuwahi kuijadili mada hii. Kwahio leo inawakilisha hatua ndogo lakini ya kihistoria," amesema balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power.

Samantha Power
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha PowerPicha: Burton/Getty Images

Power ameongeza kwa kusema, wakati umefika. Miaka 70 baada ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa, hatima ya mashoga wanaohofia maisha dunia nzima sasa inajadiliwa.

Jessica Stern, mkurugenzi mtendaji wa tume ya kimataifa ya kutetea haki za mashoga na wasagaji ameliambi baraza hilo kwamba mahakama za kundi la IS nchini Iraq na Syria wamekiri kuwaadhibu wanaojihusisha na matendo ya ulawiti kwa kuwapiga mawe, kuwauwa kwa kuwapiga risasi, kuwakata vichwa na pia kwa kuwavurumisha wavulana kutoka katika majengo marefu.

Ukatili wa IS dhidi ya mashoga

Mkutano huo ambao haukuwa rasmi uliondaliwa na Marekani pamoja na Chile, ulihudhuriwa na nchi wanachama 13 kati ya 15 wa Baraza la Usalama. Ingawa China, Urusi, Nigeria na Malaysia zilihudhuri kama wanachama wa baraza hilo, lakini hazikutoa tamko lolote. Chad na Angola hazikuhudhuria kabisa mkutano huo.

Stern amesema ni vigumu kujua mashambulizi haya yameenea kwa kiasi gani, kwasababu watu wana hofu ya kutoa taarifa zozote na kwamba chanzo kikuu cha taarifa za visa hivi ni kundu lenyewe la IS, ambalo huweka picha za watu waliyowauwa katika mtandao wa internet.

Subhi Nahas, raia wa Syria ambaye ni Shoga aliyepata hifadhi ya ukimbizi nchini Marekani ameliambia Baraza hilo kuwa mashoga, wasagaji pamoja na watu wanaozaliwa wakiwa na jinsia mbili walikabiliana na ukatili kutoka serikali ya Syria, lakini kundi la IS limeongeza makali ya ukatili dhidi ya watu hao.

Aliongeza kuwa, wakati wa mauwaji mamia ya watu wanahudhuria na kushangiria kama kwamba wapo katika sherehe ya harusi. Na kama mtu huyo bado hakukata roho baada ya kuvurumishwa kutoka katika jengo, watu wa mtaani wanampiga kwa mawe hadi anauwawa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid

Mhariri:Yusuf Saumu