1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la usalama latoa kibali cha kuwaandama maharamia Somalia.

3 Juni 2008

Vyomvo ya ulinzi wa majini vya kimataifa kuingia hadi ndani ya pwani ya Somalia kupambana nao.

https://p.dw.com/p/EBnb
Meli moja ya Uholanzi iliotekwa nyara mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu An undated handout picture of the Dutch cargo vessel Amiya Scan, which according to media reports on 27 May 2008 has been hijacked by Pirates off the Somali coast. EPA/COMM FOTO EDITORIAL USE ONLY +++(c) dpa - Bildfunk+++Picha: picture-alliance/dpa

Baraza la usalama la umoja wa mataifa, limepitisha azimio linaloruhusu vyombo vya ulinzi wa majini vya kimataifa kujiingiza katika eneo la maji la Somalia kupambana na uharamia unaofanywa dhidi ya meli zinazosafiri katika eneo hilo, jambo ambalo limesema limegeuka kuwa hatari kwa amani na usalama wa kimataifa na wa eneo hilo.

Baraza hilo la wanachama 15 linayaruhusu mataifa kutumia njia zote zinazowezekana kupambana na uharamia na wizi wa kutumia silaha katika eneo la bahari aya Somalia, jambo ambalo limekua likizidi hivi karibuni huku maharamia hao wakizikamata meli zaidi nje ya pwani ya Somalia.

Azimio hilo linaviruhusu vyombo vya ulinzi wa majini katika eneo hilo kuingia katika eneo la pwani ya Somalia kuwaandama maharamia hao kwa kutumia utaratibu utakaoheshimu sheria ya kimataifa.

Baraza hilo likatangaza kwamba vitendo vya uharamia katika pwani za Somalia na eneo la bahari nje ya pwani hizo vimegeuka kuwa kitisho kwaamani na usalama wa kimataifa katika eneo hilo, na kuitumia ibara ya 7 ya katiba ya umoja wa mataifa kuruhusu hatua za kupambana navyo, ikiwa ni pamoja na matumizi ya nguvu.

Kibali hicho ni cha muda wa miezi 6 na mataifa yametakiwa kushirikiana na serikali ya mpito mjini Mogadishu, ambayo imekiri kushindwa kuzuwia uharamia huo kwenye pwani za Somalia. Kibali hicho cha baraza la usalama kitaihusu tu Somalia .

Mwaka jana pekee kulikua na matukio 31 ya kuteka au kujaribu kuziteka nyara meli.

Katika tukio la karibuni wiki iliopita, maharamia wa kisomali waliziteka nyara meli tatu za mizigo, zilizokua zikisafiri kwa bendera ya Gibraltar, Uturuki na Uholanzi.

Azimio hilo la kupambana na uharamia katika pwani ya Somalia lilidhaminiwa na Ufaransa, Marekani, Uingereza na Panama ambayo meli nyingi husafiri kwa kutumia usajili wake. Pia nchi nyengine 12 ambazo si wanachama wa baraza la usalama, zikasaini kulipa msukumo azimio hilo, zikiwemo Japan , Korea kusini na Uhispania.