1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

090409 fußball cl bayern barca

Charo Josephat/ Hoppe, Christian9 Aprili 2009

Matumaini ya Bayern Munich kushinda kombe la Champions League yazikwa

https://p.dw.com/p/HTWR
Jogoo wa FC Barcelona Lionel Messi wa Argentina akishangilia baada ya kupachika bao la kwanza kwenye wavu wa Bayern Munich katika uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona, SpainPicha: AP

Rais wa Bayern Munich Franz Backenbauer amelaani vikali matokeo ya mechi ya jana ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya, Champions League, ambapo Bayern Munich ya Ujerumani ilicharazwa mabao 4-0 na Barcelona ya Spain kwenye mchuano uliochezwa katika uwanja wa Camp Nou mjini Barcelona. Mji wa Munich leo umeamka na huzuni huku washabiki wa Bayern wakilalamika kuhusu matokeo ya timu yao.

Franz Backenbauer, mchezaji mkongwe wa timu ya kitaifa ya Ujerumani, amesema kushindwa kwa Bayern Munich na Barcelona kwa magoli 4-0 ni wakati mgumu na wa majaribu makubwa katika historia ya Bayern. Backenbauer pia amesema mechi ya jana ni kama fedheha na kwamba Barcelona imeipa funzo Bayern katika mchezo wa kandanda.

Mabao yote manne ya Barcelona yalifungwa katika kipindi cha kwanza cha ngoma iliyochezwa katika uwanja wa Camp Nou huko Barcelona, ikiwa ni raundi ya kwanza ya robo fainali ya kuwania kombe la Champions League. Lionel Messi aliutikisa wavu wa Bayern mara mbili huku Samuel Eto´o na Thiery Henry wakipachika goli moja kila mmoja.

Mwenyekiti wa timu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge, amekiri kwamba matumaini ya timu hiyo kushinda kombe la Champions League yamezikwa.

"Leo tumeshuhudia siku ambayo mtu anaweza kuieleza kuwa aibu kubwa mno. Kwa mchezo huu ni wazi kwamba tumetoka kwenye mashindano ya klabu bingwa barani Ulaya. Hilo liko wazi kabisa. Sasa lazima bila shaka tuokoe kila tunachoweza kuokoa katika ligi ya Ujerumani, Bundesliga. Hilo nalo ni jambo lilo wazi."

Deutschland Fußball Jürgen Klinsmann neuer Trainer bei Bayern München
Kocha wa Bayern Munich Juergen Klinsmann (kulia) na rais wa timu hiyo Karl-Heinz RummeniggePicha: AP

Karl Heinz Rummenigge lakini amekataa kuzungumzia kuhusu hatima ya kocha wa Bayern, Jurgen Klinsmann na badala yake kusisitiza umuhimu wa kushinda mechi ijayo dhidi ya Frankfurt siku ya Jumamosi. "Lazima tushinde baada ya kushindwa vibaya namna hii kwa mara ya pili mfululizo," amesema Rummenigge.

Kushindwa kwa Bayern na Barcelona kunafuatia kushindwa na timu ya Wolfburg kwa mabao 5-1 kwenye mechi ya Bundesliga mwishoni mwa juma lililopita.

Bayern ilicheza bila wachezaji wake muhimu waliokuwa na majeraha lakini, meneja wa timu hiyo, Uli Hoenness anasema hiyo si sababu ya kutosha ya kufungwa mabao manne na Barcelona.

"Hilo kwa hakika limechangia, lakini jinsi tulivyocheza katika kipindi cha kwanza cha mchezo swala la kukosekana wachezaji wanne muhimu kwenye timu linaweza kuwekwa kando."

Kilio mjini Munich

Mji wa Munich leo umeamka na huzuni huku washabiki wa Bayern wakilalamika kuhusu matokeo ya timu yao. Washabiki wa Bayern Munich wamehuzunishwa sana na matokeo ya timu yao. Mmoja wao ni Malumbo, mtanzania anayeishi mjini Munich.

"Kusema kweli jana mpira ambao walicheza Bayern si mpira mzuri kama ule wanaocheza kila siku kutokana na kwamba baadhi ya wachezaji wao muhimu hawakucheza kama vile Lamm, Mbrazil Lucio na Mbelgium, watu ambao wanategemewa sana katika timu yao. Ni huzuni kubwa na inamuweka sehemu mbaya sana kocha wao wa sasa hivi Jurgen Klinsmann."

Akiieleza hali ilivyo katika barabara za mji wa Munich hii leo, Malumbo anasema,"Hali ya washabiki sasa hivi ni ya kusikitisha sana. Washabiki wengi wamenyong´onyea kwa sababu matokeo ya jana watu wengi hawakutegemea. Walitegemea labda Bayern watashinda au watoka suluhu, lakini matokeo ya jana magoli 4:0 kwa timu kama Bayern ni mabao mengi sana kwa timu kama ile."

Malumbo ameongeza kuwa kwamba ijapokuwa wachezaji wa Bayern Munich walijitayarisha kwa muda mrefu kwa mechi kama hii, wamefungwa mabao mengi na yanasikitisha. Mambao hayo yanavunja hata matumaini kwamba mecho ya mrudiano wataweza kurudisha mabao kama yale."

Chelsea yainyoa Liverpool bila maji

Katika mechi nyingine ya Champions League, Chelsea iliishangaza Liverpool kwa kuitandika mabao 3-1 huko Anfield. Fernando Torres alipachika bao la kwanza la Liverpool dakika ya sita baada ya mchuano kuanza, lakini Branislav Ivanovic akakomboa kwa Chelsea dakika ya 39. Alifunga balo la pili la Chelsea dakika ya 62 na hatimaye Didier Drogba akaukomelea msumari wa mwisho kwenye jeneza la Liverpool dakika tano baadaye.

Fußball Champions League FC Liverpool Rafael Benitez
Kocha wa Liverpool Rafael BenitezPicha: AP

Kocha wa Liverpool Rafa Benitez amesema mechi ya raundi ya pili itakuwa ngumu na wanalazimika kuifunga Chelsea mabao 3 lakini anaamini wataweza kufanya hivyo.