1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barua kutoka Dar

11 Mei 2016

Watanzania wengi hawana ndoto ya kwenda kufanya kazi ughaibuni, kuepukana na umaskini. Lakini mwandishi Anaclet Rwegayura anahoji, iwapo uchumi wa taifa hilo unaweza kufikia tabaka la kati.

https://p.dw.com/p/1IlgF
Tansania Budget
Picha: DW/Kizito Makoye Shigela

Mafundi na wote wafanyao kazi za sulubu katika nchi hii wanaendelea na shughuli zao za kawaida bila hata chembe ya tamaa kwamba siku moja wangehesabiwa miongoni mwa matajiri au wafanyabiashara wakubwa. Lengo lao ni kuweka maisha yao katika usawa na ulimwengu.

Sehemu ndogo ya watu inayopata fursa ya ajira, aghalabu katika maeneo ya mijini, hutaka wawe na kipato cha hakika. Kwa desturi, wakazi wa vijijini walifaidika kwa njia mbalimbali kwa kuwa na jamaa zao waliobahatika kupata ajira mijini. Ulikuwa mfumo mzuri wa maisha wenye wafanyakazi wakaao mijini wakifadhili ustawi wa familia za vijijini na maendeleo ya vijijii vyao.

Hivi karibuni, hata hivyo, hali hiyo imekuwa shaghalabaghala. Mahusiano ya kiuchumi yaliyokuwepo kwa muda mrefu kati ya familia za vijijini na wafanyakazi waishio mijini imebadilika ghafla kila upande ukijizatiti peke yake ili uendelee kuishi.

Jamii za vijijini zimeathirika sana kutokana na kupungua kwa mazao yauzwayo nchi za nje kama vile kahawa, chai, pamba, korosho, nyama na mengine mengi kutokana na, baadhi ya sababu, kushindwa kwao kukidhi matakwa ya ushindani wa masoko ya kimataifa.

Mazao mengi bado hayajafikia viwango vilivyowekwa, ikiwa pamoja na vya kulinda afya za walaji, usafi na usalama ili viweze kupata hati za kuruhusiwa viingizwe, kwa mfano, katika soko la Ulaya.

Kiwango kidogo cha mapato ya mazao yauzwayo nje ya nchi, hasa kutokana na sekta ya kilimo, yanamaanisha uwezo mdogo wa serikali na hata sekta binafsi kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Hali hii itakuwa ngumu zaidi kutokana na urahisi wa watafuta ajira kuhama katika nchi sita wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Katika ujumbe unaotangazwa kila siku na vituo vya televisheni, Rais John Pombe Magufuli anawahimiza Watanzania wawe na tabia ya kulipa kodi katika shughuli zote za biashara na mapato.

Tansania Präsident John Magufuli
Rais wa Tanzania John Pombe MagufuliPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Akihutubia kwa mara ya kwanza mkutano wa hadhara wa Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka huu, Rais Magufuli alitamka: “Nchi yetu haitaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uvivu, uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji kodi, kutotimiza wajibu wetu na wafanyakazi hewa.“

Maovu yote haya, kama hayakuachwa, yatamaliza uchumi na kupeleka nchi katika hali ya kugutusha. Hakuna mtu atakuwa na fursa ya kuwa na kipato kizuri na endelevu. Wafanyakazi wengi hawatakuwa na muda wa mapumziko, kutunza maisha ya familia zao na hata michezo ambayo husaidia kutunza afya zao kimwili, kimawazo na kisaikolojia.

Katika baadhi ya nchi ambazo, kwa bahati mbaya, zimekuwa na uongozi usiofaa, vizazi vimesambaratika kutokana na uchumi duni. Je, ni Watanzania wangapi wanatambua hilo?

Hotuba ya rais ilimfanya kila mfanyakazi afumbe na kufumbua jicho baada ya kuwapunguzia asilimia 2 katika kodi inayokatwa katika mishahara yao kuanzia Mei 2016.

Lakini agizo hilo la rais halikufunga mjadala katika asasi mbalimbali juu ya kiwango gani cha mshahara kinastahili kwa maisha ya mfanyakazi katika mazingira yanayobadilika ya uchumi wa dunia ambapo umaskini unaendelea kuwa adui asiyekamatika kwa Watanzania.

Wakati huu, nchi inakabiliwa na udhaifu na vikwazo vingi ambavyo vinatishia ukuaji wa uchumi.

Mbali ya kupambana na ufisadi, uboreshaji wa kuonesha matokeo ya kazi za serikali na kuhimiza utawala wa sheria, miongioni mwa mambo mengine, hapana budi vyama vya wafanyakazi vishirikishwe kikamilifu pamoja na waajiri na bodi za mazao kutathmini tofauti za mishahara na kuwezesha wazalishaji na wafanyakazi wawe na tija ya juu kabisa.

Mwandishi: Anacleti Rwegayura

Mhariri. Iddi Ssessanga