1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern haitikisiki, Dortmund bado hoi

15 Desemba 2014

Bayern Munich imeikamilisha wikendi ikiongoza na pengo la points tisa katika msimamo wa Bundesliga, baada ya nambari mbili Wolfsburg kutekwa kwa sare ya goli moja kwa moja nyumbani na Paderborn

https://p.dw.com/p/1E4Ma
Medhi Benatia 13.12.2014 Bayern vs Augsburg
Picha: Reuters/M. Rehle

Beki wa Paderborn Rafel Gomez alijifunga goli langoni mwake na kuwapa Wolfsburg uongozi kabla ya kipa wa Paderborn Lukas Kruse kuokoa mkwaju wa penalty wake Ivan Perisic. Kiungo wa Paderborn Alban Meha alifunga penalty na kuisawazishia timu yake. Kocha wa Wolfsburg Dieter Hecking alikiri baada ya mchuano kuwa walishindwa kupata points zote tatu kwa sababu ya mlinda lango wa Paderborn Lukas Kruse aliyefanya maajabu langoni. Elias Kachunga ni shambuliaji wa Paderborn

Katika mchuano wa mapema jana, Bayer Leverkusen na Borussia Moenchengladbach ziligawana point moja kila mmoja baada ya kutoka sare ya kufungana goli moja kwa moja ili kusonga katika nafasi ya tatu na nne kwenye msimamo wa ligina pengo la points sita nyuma ya nambari mbili Wolfsburg.

Bundesliga 13.12.2014 Berlin gegen Dortmund
Kocha wa Borussia Dortmund anastahili kutafuta suluhisho la matokeo duni ya vijana wakePicha: Reuters/Bensch

Wenyeji Leverkusen walikuwa wa kwanza kutikisa wavu kupitia kiungo Mturuki Hakan Calhanoglu kabla ya Gladbach kusawazisha kupitia beki Mholanzi Roel Brouwers.

Bayern walisalia usukani baada ya kuwabwaga Augsbrug mabao manne kwa sifuri matokeo ambayo yamewafanya Augsburg kudondoka kutoka nafasi ya tatu hadi ya tano. Arjen Robben alifunga mawili huku Medhi Benatia na Robert Lewandowski wakifunga moja kila mmoja.

Wakati Bayern ikiendelea kupepea, timu inayowafanya mashabiki kujiuliza maswali ni Borussia Dortmund ambao wamerudi katika nafasi za kushushwa daraja baada ya kufungwa goli moja kwa sifuri na Hertha Berlin. Hicho ni kichapo cha Dortmund cha tisa katika mechi 15 za ligi ambacho kimewateremsha kutoka nafasi ya 14 hadi 16 baada ya kuanza mwezi wa Desemba wakishikilia mkia. Julian Shchieber alifunga goli hilo la ushindi dhidi ya timu yake ya zamani, na kufanya mambo kuwa mabaya hata zaidi, kiungo wa BVB Heinrikh Mkhitaryan amepata jeraha litakalomweka nje kwa kipindi cha wiki sita. Huyu hapa kocha Jurgen Klopp

Ni matokeo ya sare ya magoli matatu kwa matatu kati ya Hanover na Werder Bremen yaliyoizuia Dortmund kubingiria katika nafasi ya pili kutoka nyuma. Schalke waliduwazwa na FC Cologne kwa kufungwa mabao mawili kwa moja. Hamburg walikabwa kwa sare ya kutofungana goli na Freburg na timu zote ziko katika eneo la mkia. Hoffenheim ilipata ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Eintracht Frankfurt ili kusalia katika nafasi ya saba ya ligi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters
Mhariri: Yusuf Saumu