1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kuendelea kuvunja rekodi zaidi

28 Machi 2014

Huku tayari taji la Bundesliga likiwa mikononi mwao, Bayern Munich wanaweza sasa kuanza kufikiria kuumaliza msimu bila kushindwa mchuano wowote huku pia wakijikusanyia pointi nyingi katika ligi ya nyumbani.

https://p.dw.com/p/1BYA3
Fußball Bundesliga - Der FC Bayern München ist Meister
Picha: Getty Images

Borussia Dortmund na Schalke zinagombania nafasi ya pili huku mapambano ya kuepuka kushushwa daraja yakizihusisha timu saba ikiwa ni pamoja na mabingwa wa zamani Stuttgart na Hamburg.

Bayern, ambao ndio mabingwa wa mapema zaidi katika historia ya Bundesliga, huenda wakavunja rekodi yao ya msimu uliopita ambao walimaliza na points 91. Sasa wana 77, huku ikisalia mechi saba pamoja na points 21 za kukusanya. Bayern wameshinda mechi 25 kati ya 27, na kutoka sare mara mbili pekee. Wameshinda mechi zao 19 za mwisho katika Bundesliga na hawajashindwa katika mechi 52. Na sasa vijana hao wa Pep Guardiola wanalenga kunyakua mataji matatu muhimu kama walivyofanya msimu uliopita..yaani Bundesliga, Champions League na Kombe la Shirikisho Ujerumani.

Huyu hapa kocha Pep baada ya kunyakua taji lao la 24 la Bundesliga "Tumefurahishwa sana kuwa mabingwa wa Ujerumani. Bayern imetetea taji lao. Shukrani kwa fursa niliyopewa kuwa hapa na kuwafunza wachezaji hawa mahiri. Hongera kwa kikosi kizima. Mmenipa heshima kubwa na kunionyesha ari kubwa. Katika msimu huu, tumeshinda mechi nyingi sana. Na bila shaka huu ni ushindi wa Uli Hoeness, ambaye ni mtu muhimu kabisa katika klabu hii. Tumefaulu na kucheza vyema. Bila shaka Nimefurahishwa sana na taji hili".

Pep Guardiola ametwaa taji la Bundesliga katika msimu wake wa kwanza Ujerumani
Pep Guardiola ametwaa taji la Bundesliga katika msimu wake wa kwanza UjerumaniPicha: Bongarts/Getty Images

Mkurugenzi wa spoti wa klabu ya Bayern Mathias Sammer alimmiminia sifa Pep kutokana namafanikio hayo. "Kwa kweli mambo yanaonekana kuwa rahisi, lakini ukweli pia ni kuwa kwa kocha kuhamia hapa msimu huu na kuwa na msimu wenye mafanikio inadhihirisha uwezo mkubwa ambao anao Pep Guardiola na wachezaji wetu".

Mlinda lango Manuel Neuer anasema baada ya ushindi huo sasa wanauangazia mchuano unaofuata. "Bila shaka ni furaha kubwa. Tulijitahidi sana, na kwa kweli kila juhudi tulizofanya zimwetupa ubingwa wa Ujerumani. Kupata ubingwa mapema hivyo, imetushangaza lakini tuna furaha na tunalenga mbele"

Bayern wamekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu na hata ushindi wao umepokea pongezi kutoka kwa mpinzani wao mkubwa, Borussia Dortmund. Huyu hapa kocha wa BVB Jurgen Klopp. "Mwendelezo wao walioonyesha ni wa ubora wa hali ya juu, ambao ni mfano mzuri. Wamestahili kuchukua ubingwa mapema sana. Hilo linastahili pongezi. Hivyo twawavulia kofia. Heshima kubwa. Hongera". Borussia Dortmund wako mbele ya Schalke na faida ya point moja katika vita vya kuwania nafasi ya pili. Bayer Leverkusen saa wako katika nafasi ya nne na wanaonekana kuwa timu ya mwisho kujikatia tikiti ya kucheza katika Champions League.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Yusuf Saumu