1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern mabingwa wa Bundesliga 2013

7 Aprili 2013

Bayern Munich, wameshinda taji lao la 23 la Ligi ya soka Ujerumani – Bundesliga na kuweka rekodi ya kuwa washindi wa mapema kabisa wa Ligi kuwahi kushuhudiwa Ujerumani zikiwa zimesalia mechi sita msimu kukamilika

https://p.dw.com/p/18B6M
FRANKFURT AM MAIN, GERMANY - APRIL 06: Bastian Schweinsteiger of FC Bayern Muenchen celebrates scoring the opening goal with team mate Dante during the Bundesliga match between Eintracht Frankfurt and FC Bayern Muenchen at the Commerzbank-Arena on April 6, 2013 in Frankfurt am Main, Germany. (Photo by Alex Grimm/Bongarts/Getty Images)
Bundesliga Tor Jubel FC Bayern München Dante SchweinsteigerPicha: Bongarts/Getty Images

Sasa Bayern wamesalia na mechi sita wakiandaa gwaride la kulionyesha taji la Bundesliga, baada ya kiungo Bastian Schweinsteiger kufunga bao la kiustadi kwa njia ya kisigino na kuwapa ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Eintracht Frankfurt.

Vijana hao wa Mkufunzi Jupp Heynckes wamemaliza uongozi wa miaka miwili wa Borussia Dortmund kwa kushinda taji la 22 la Bundesliga mapema kuliko klabu nyingine yoyote katika historia ya miaka 50 ya ligi hiyo. Bayern walikosa nafasi baada ya Xherdan Shaqiri kuupiga mlingoti wa goli, wakati David Alaba akikosa kufunga mkwaju wa penalti. Ushindi huo uliwapa Bayern uongozi wa jumla ya pointi 75

Kocha wa Bayern Jupp Heynckes amewapongeza vijana wake kwa kuwa na mshikamano msimu huu
Kocha wa Bayern Jupp Heynckes amewapongeza vijana wake kwa kuwa na mshikamano msimu huuPicha: Reuters

Jupp Heynckes amesema ni vizuri sana kushinda tena taji baada ya miaka 23. aliwaongoza Bayern kutwa mataji ya mwaka wa 1989 na 1990 wakati akiwa kocha. Heynckes atampisha Mhispania Pep Guardiola mwishoni mwa msimu huu wakati ambapo Bayern huenda watakuwa wameongeza mataji mengine mawili, Champions League na Kombe la Shirikisho. Nahodha wa Bayern Philip Lahm anasema sasa wameangazia macho yao katika mchuwano wa marudio wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Juventus.

Dortmund yatoka nyuma dhidi ya Augsburg

Nambari mbili Dortmund, ambao walifanya mabadiliko saba katika kikosi ambacho kilitoka sare ya bila kufungana na Malaga katika mchuwano wao wa Champions League, walifanya kazi kubwa kupata ushindi wa magoli manne kwa mawili dhidi ya klabu inayochungulia kaburi la kushushwa daraja Augsburg. Mshambuliaji wa Dortmund Julian Schieber alifungua ukurasa wa magoli kabla ya Augsburg kuamka na kumiliki mpira kipindi kizima cha kwanza, wakati Daniel Baier akisawazisha kabla ya Kevin Vogt kuongeza la pili muda mfupi baadaye. Kisha kocha Jurgen Klopp akaongeza mashambulizi katika kipindi cha pili kwa kumleta Robert Lewandoswki na Mario Goetze. Mabadiliko hayo yalisababisha goli kutoka kwa Julian Schieber, Neven Subotic, kabla ya Lewandowski kufunga kazi katika dakika ya mwisho.

Mshambuliaji chipukizi wa Dortmund Julian Schieber alitikisa mara mbili nyavu za Augsburg
Mshambuliaji chipukizi wa Dortmund Julian Schieber alitikisa mara mbili nyavu za AugsburgPicha: AFP/Getty Images

Leverkusen yakabwa na Wolfsburg

Bayer Leverkusen iliweza tu kupata sare ya goli moja kwa moja nyumbani dhidi ya nambari 12 Wolfsburg matokeo ambayo yalikuwa pigo kubwa katika juhudi zao kujiunga na Dortmund katika nafasi ya pili. Andre Schürrle alifunga goli la Leverkusen wakati Simona Kjaer akiwasawazishia Wolfsburg katika dakika ya 70.

Schalke iliizidi nguvu Bremen ugenini baada ya kipindi kibovu cha kwanza kilichokosa msisimko
Schalke iliizidi nguvu Bremen ugenini baada ya kipindi kibovu cha kwanza kilichokosa msisimkoPicha: Bongarts/Getty Images

Schalke yaiadhibu Bremen

Katika msimu mwingine, mchuwano baina ya Schalke na Bremen ungekuwa mpambano wa kuwania nafasi ya nne bora. Lakini mechi ya jana Jumamosi ulikuwa tu mpambano kati ya Schalke nambari nne wa ligi na Bremen ambao waki katika nafasi ya 14. Julian Draxler aliwapa Schalke uongozi kabla ya Ciprian Marica akinufaika na masihara yaliyofanywa na beki wa Bremen Assani Lukimya kwa kugonga pasi mbovu ya nyuma….

Kwingineko Borussia Moenchengladbach walipata ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya klabu inayoshikilia mkia Greuther Fürth, bao lililofungwa na Luuk de Jong.

Hamburg yaduwazwa nyumbani na Freiburg

Katika mechi iliyochezwa jioni, nambari nane katika ligi Freiburg walisafiri kucheza ugenini kwa nambari tisa Hamburg na wakarudi kwao na ushindi wa bao moja kwa sifuri.

Mwandishi. Bruce Amani/DW

Mhariri: Iddi Sessanga