1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich au Inter Milan kutwaa vikombe 3

17 Mei 2010

Marekebisho ya Kalenda ya Kombe la Afrika la mataifa 2013

https://p.dw.com/p/NQH0
Mark van Bommel -nahodha wa B.Munich na Kombe la pili.Picha: AP

Bayern Munich, imeipelekea salamu kali Inter Milan ya Italy juzi Jumamosi ilipoikomea Werder Bremen, mabao 4:0 na kutwaa Kombe la Ujerumani na sasa inalitaka kombe la 3 la Champions League wiki ijayo.

Inter Milan nayo, imezirudisha kwa Bayern Munich, salamu hizo hizo ilipoilaza Jumapili Siena kwa bao 1:0 na kutwaa tena taji la ubingwa wa Italy na Kombe la pili msimu huu kama ilivyofanya Munich.

Wiki 3 hivi zikisalia kabla ya Kombe la dunia, nchini Afrika kusini, nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack, ameumia.

BAYERN MUNICH DHIDI YA INTER MILAN:

Ijumamosi ijayo Bayern Munich au Inter Milan , mojawapo yaweza kumaliza msimu huu kwa kutwaa vikombe 3-viwili nyumbani na 1 cha mabingwa wa Ulaya- Champions League na hivyo, kuandika historia mjini Madrid.Mei 22:

Mdachi Arjen Robben , alilifumania lango la Bremen katika kipindi cha kwanza kwa bao la mkwaju wa penalty. Ribery na Bastian Schweinsteiger , kila mmoja akitia bao lake katika kipindi cha pili cha mchezo.

Werder Bremen, ilimaliza mchezo na wachezaji 10 tu uwanjani baada ya nahodha wao, Torsten Frings, kutimuliwa nje ya uwanja mnamo dakika ya 76 ya mchezo kwa kucheza ngware.

Baadae kocha wa Bayern Munich, mdachi Van Gaal, alisema kuwa timu yake ilicheza uzuri sana dhidi ya adui mkali. Akaongeza kusema kwamb, aonavyo yeye ulikuwa ndio mchezo bora kabisa timu yake iliocheza msimu huu.

Aliwaambia wachezaji wake ni muhimu kushinda, lakini vipi pia kuufikia ushindi huo. Bremen, ingestahiki kuongoza katika dakika ya 8 ya mchezo pale mshambulizi wake, Claudio Pizarro, alipojikuta pekee na kipa wa Bayern Munich ,Joerg Butt.

Ushindi wa Kombe la Ujerumani wa Bayern Munich, katika uwanja wa Olimpik wa Berlin, umekuja wiki tu baada ya kuvaa taji la ubingwa katika uwanja huo huo kwa kuwazaba wenyeji, Hertha Berlin, mabao 3:1.

Sasa Bayern Munich, inasubiri kutekeleza miadi yake Jumamosi ijayo mjini Madrid itakapocheza na mabingwa wa Italy,Inter Milan, kuania kila mmoja taji lake la 3 msimu huu. Inter jana iliikomea Siena, bao 1:0 na kuvaa taji la Italy baada ya kutwaa Kombe la Taifa. Swali linaloulizwa sasa : ni nani kati ya Kocha Van Gaal wa Bayern Munich na Louis Mourinho wa Inter Milan ,atakuja na mbinu za kumuangusha mwenziwe huko Madrid ?

Kwa Mourinho, taji la Inter Milan, jana ni taji lake la 6 alizozivalisha klabu mbali mbali za Ulaya: Aliitawaza FC Porto ya Ureno, mabingwa mara 2 na mara 1 hata mabingwa wa Ulaya. Halafu akaitawaza Chelsea, mabingwa wa Premier League mara 2 nchini Uingereza.

Wakati FC Barcelona, ikitamba na Lionel Messi wa Argentina , ilitoroka jana na taji la ubingwa la Spain kwa mara nyengine tena, Chelsea, imeigiza Bayern Munich na Inter Milan, kutwaa vikombe 2 nyumbani msimu huu.

Chelsea,ilizima vishindo vya Portsmouth, inayorudi msimu ujao daraja ya pili kwa kufilisika kifedha, lakini sio kidimba. Chelsea, kutokana na bao maridadi la nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba katika Uwanja wa Wembley, ilimaliza msimu huu kwa vikombe 2 na kuiacha Manchester united, imetoka mikono mitupu.

Katika finali hii ya kwanza kati ya mabingwa waliopo kileleni na timu ya mkiani-Portsmouth, Chelsea, ilitamba kipindi cha kwanza, lakini mara 5 hujuma zao katika lango la Portsmouth zilishindwa kufua dafu: Drogba mara mbili, Frank Lamperd mara 1, Salomon Kalou mara 1 na John Terry 1-wote waligonga mwamba wa lango la Portsmouth.

MICHAEL BALLACK AMEUMIA :

Katika finali hiyo ya kombe la FA, nahodha wa Ujerumani, Michael, Ballack, akiichezea Chelsea Jumamosi, alichezewa ngware na mghana, Boateng wa Portsmouth. Baada ya ukaguzi wa kitibabu aliofanyiwa leo mjini Munich, na daktari wa Timu ya taifa, Hans-Wilhelm Müller-Wohlfahrt, imebainika kwamba, Ballack, hataweza kuiongoza Ujerumani katika kombe lijalo la dunia. Hii imearifu leo, Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) mjini Frankfurt.

Ballack, anaweza kupona kikamilifu, iliarifu DFB, lakini hii itachukua wiki 8 hadi atakapoweza Ballack kuanza mazowezi. Hili ni pigo la pili baada ya kipa wa Taifa Rene Adler wa Bayer Leverkusen kuumia.

Ujerumani, imepangiwa kuanza dimba katika kundi lake na Australia hapo Juni 13. Ilipangwa mara tu baada ya kujua matokeo ya uchunguzi wa X-ray aliofanyiwa leo, angemuarifu kocha Löw huko Sicily, Italy, ambako Ujerumani imepiga kambi yake ya mazowezi kwa Kombe la dunia.Ujerumani, itacheza na Ghana katika kundi D nchini Afrika Kusini.

Ballack alisema baada ya kupigwa teke na mghana Boateng wa Portsmouth :

"Alinipiga teke vibaya sana .Tumejionea katika TV na sijui alifanya kusudi, lakini natumai hajakusudia...."

Kocha wa Ujerumani, Joachim Löw, akielezea matumaini kwamba, nahodha wake pengine hakuumia vibaya na baada ya kuugua kidogo angejiunga na timu ya Ujerumani kwa kombe la dunia alisema:

"Natumai kesho tutapata habari itakayotufurahisha sote. Ballack atahitaji siku chache za kujiuguza na mwishoe, natumai kila kitu kitakua barabara."

Kocha Joachim Löw, alikosea. Ujerumani itabidi kucheza bila nahodha wake na bila ya nahodha, tutumai jahazi la Ujerumani huko Afrika Kusini,halitaenda mrama seuze kuzama.

Ballack ameichezea Ujerumani mara 98 na ametia mabao 42 kwa timu ya taifa na alitazamiwa kuiongoza Ujerumani Afrika kusini kutwaa Kombe lake la 4 la dunia. sasa ,Ujerumani itabidi kusaka nahodha mwengine:Je, nani huyo ?

Maoni mbali mbali yametolewa kuhusu kuumia kwa nahodha wa Ujerumani: Kocha wa zamani wa Taifa, Berti Vogts, alisema kwamba, kuumia nahodha Ballack, ni pigo kubwa kwa Ujerumani. Anatumai kuwa, Bastian Schweinsteiger, sasa atajaza pengo hilo. Rudi Völler-kocha wa zamani wa taifa na mshambulizi, alisema, ni msiba mkubwa kuumia Ballack. " Alikuwa na matumaini makubwa na alipanga kutia fora mno katika Kombe hilo la dunia" -alihuzunika Rudi Völler, mkurugenzi wa Bayer Leverkusen.

Wakati kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati, kilianza mjini Kigali,Rwanda mwishoni mwa wiki, na Tanzania ikiwakilishwa na Simba upande wa Tanzania-bara na Mafunzo kwa Zanzibar, Taifa Stars, timu ya taifa, inaingia kambini kesho kujiandaa kwa duru yake ya pili na Ruanda, kuania tiketi ya kushiriki katika Kombe la Afrika kwa wachezaji wa nyumbani:

KOMBE LA AFRIKA:

Kombe la Afrika la mataifa: Kuanzia mwaka 2013 Kombe la Afrika la Mataifa litaaniwa mwaka mwengine kinyume na kalenda ya hadi sasa. Hii ni kwa muujibu wa vile CAF-Shirikisho la dimba la Afrika lilivoamua jana mjini Cairo. Hii ina maana kutafanyika mapambano 2 mwaka 2012 na tena mwaka 2013: Guinea ya Ekweta na Gabon, zitaanda kwa ubia 2012 na Libya mwaka utaofuatia 2013.

Libya, imekubali kuandaa Kombe hilo la Afrika 2013 ili kuiwezesha CAF kuandaa Kombe hilo mwaka usio wa kawaida. Rais wa CAF, Issa Hayatou, hakutaja lakini, mabadiliko ya wakati wa kuchezwa Kombe la Afrika badala ya mwanzo wa mwaka na kuchezwa Juni au July. CAF , imearifu pia kinyan'ganyiro cha kuania wapi Kombe la Afrika lianiwe 2015 na 2017 kitaanza karibuni.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE/AFPE

Imepitiwa na Hamidou Oummilkheir