1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich itafaulu mbele ya Chelsea?

19 Mei 2012

Swali ni iwapo Bayern Munich baada ya kujeruhiwa katika ligi na kombe la shirikisho DFB Pokal, watakuwa na uwezo wa kupambana na FC Chelsea na kulibakisha kombe la Champions League nyumbani.

https://p.dw.com/p/14ybO
---
Hiyo ndio miamba inayokodolewa macho jioni ya leo katika fainali Bayern München Chelsea FC

Chelsea imewasili katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria , Munich wakiwa na shauku ya kumaliza muda mrefu wa kusubiri kuvishwa taji la wafalme wa soka katika bara la Ulaya katika uwanja wa Allianz Arena mjini Munich, miaka minne baada ya kushindwa katika fainali iliyofanyika mjini Moscow .

Die Allianz-Arena in München (Oberbayern) leuchtet am Montag (14.05.2012) in den Farben Grün, Blau und Türkis. Während des Finales der Champions League lässt die UEFA das Stadion in den ungewohnten Farben erstrahlen. Am Samstag (19.05.2012) empfängt der FC Bayern München den FC Chelsea zum Finale der Champions-League in der heimischen Arena. Foto: Sven Hoppe dpa/lby +++(c) dpa - Bildfunk+++
Huo ndio uwanja wa Allianz Arena unapigiwa fainali hiyoPicha: picture-alliance/dpa

Mara ya mwisho Chelsea kufikia fainali ya Champions League ni mwaka 2008 ambapo timu hiyo ilipoteza mchezo huo dhidi ya Manchester United , walipoteza kwa mikwaju ya penalti huku mshambuliaji wao nyota Didier Drogba akitolewa nje kwa kadi nyekundu katika muda wa nyongeza baada ya kumlamba kibao mlinzi wa United Nemanja Vidic.

Licha ya kuwa na msimu uliokuwa wa kuyumba yumba ambapo Chelsea ilimaliza ikiwa ya sita katika ligi ya Uingereza , Premier League , Chelsea ilifanikiwa kunyakua taji la kombe la FA na kuishinda Barcelona katika njia yao kuelekea katika fainali hii ya Champions League mjini Munich.

Chelsea ina matumaini

Baada ya kocha Andre Villa-Boas kufutwa kazi kama meneja wa timu hiyo mwezi March, bosi mpya Roberto Di Matteo amefanikiwa kuleta uhai katika timu hiyo na Drogba anasema Chelsea ina haki ya kufika pale ilipo hivi sasa. Kocha mlezi wa Chelsea Roberto Di Matteo anaelezea matumaini yake.

"Nafikiri mchezo huu unaweza kuamua historia ya club yetu, kwasababu itakuwa mara ya kwanza ambapo tutaweza kubeba kombe hili, na hilo ndio muhimu na lengo letu kwa sasa."

Kwa upande wake winga wa kulia wa Bayern Munich Frank Ribery anafahamu machungu ya kushindwa kushiriki katika fainali ya mwaka 2010, ambapo kadi nyekundu aliyopewa wakati wa mchezo wa nusu fainali kati ya timu yake na Olympique Lyon, ilisababisha kutoshiriki katika mchezo wa fainali ambapo Bayern Munich ilipoteza mchezo huo kwa mabao 2-0 dhidi ya Inter Milan mjini Madrid.

Baada ya dhiki faraja

Vigogo hao wa soka kutoka Bavaria wamekwisha fikia fainali mara mbili kati ya tatu zilizopita , na Frank Ribery ana shauku ya kulinyakua taji hilo baada ya kulikosa miaka miwili iliyopita.

Mshambuliaji wa pembeni wa vigogo hao wa Bayern Munich, Arjen Robben amesema machungu ya kushindwa kupata mafanikio katika ligi ya nyumbani na kombe la shirikisho DFB Pokal ,yanatoa changamoto kwao kulinyakua kombe hilo hii leo.

"Kwa kipigo tulichokipata katika kombe la shirikisho pamoja na kupoteza tena ubingwa wa ligi, bado kuna nafasi ya kunyakua taji la mwisho msimu huu, na nafikiri , kuwa hali hii inaweza kutupatia motisha zaidi kuweza kupata ushindi leo Jumamosi".

Kizazi cha dhahabu

Majina ya kina Franz Beckenbauer, Gerd Mueller na Oliver Kahn yana umaarufu wa kimiujiza katika mji mkuu wa jimbo la Bavaria , Munich na kwingineko nchini Ujerumani. Ubingwa mara tatu mfululizo wa kombe la Ulaya katika miaka ya 70 umemuinua rais wa heshima wa Bayern Munich Beckenbauer na wachezaji wenzake na kuwaweka katika vitabu vya historia nchini humo.

Ukijumlisha hayo yote pamoja na ubingwa wa dunia wakiwa na timu ya Ujerumani magharibi wakati huo , rekodi yao inaonekana kuwa bora zaidi. Ushindi wa Bayern wa Champions League katika mwaka 2001, miaka miwili baada ya kushindwa na Manchester United , ulisababisha mashabiki wa club hiyo kumvisha mlinda mlango wao maarufu Oliver Kahn , jina la utani la Titan.

Hata hivyo kushindwa dhidi ya Chelsea katika fainali hii ya Champions League leo Jumamosi , kutawavua wachezaji wa sasa wa Bayern haki ya kuitwa kizazi cha dhahabu, amesema nahodha wa timu hiyo Philipp Lahm. Hata kama kikosi hiki kina vipaji vya hali ya juu kabisa , bila ya ushindi ni kazi bure, amesema Lahm.

Kila enzi kuu inapambwa na mataji, Lahm amewaambia waandishi habari wiki hii.

Frank Lampard, der Pokal und Mario Gomez --- DW-Grafik: Peter Steinmet
Nahodha wa Chelsea FC , Frank Lampard na Mshambuliaji wa FC Bayern Mario GomezPicha: AP

Iwapo hakuna mafanikio ya kuleta vikombe, kizazi hiki hakitazungumziwa kabisa, hata kama kina vipaji vya hali ya juu, na hakuna mtu atakayezungumzia , enzi za kizazi cha dhahabu, hivi ndivyo ninavyojipima, ameongeza Lahm.

Ni kama ndoto ya mchana

Wachezaji wa Chelsea hawakutarajia kufikia kucheza katika fainali ya mwaka huu, amesema nahodha wa muda Frank Lampard .Lampard ambaye anashikilia wadhifa wa nahodha kutokana na John Terry kuwa na kadi nyekundu na kushindwa kushiriki katika fainali hiyo amesema wachezaji wa Chelsea wasingeamini kuwa wangekuwa hapa walipo hivi sasa katika fainali. Tunafuraha sana kuwa hapa tulipo, lakini miezi michache iliyopita , hatukutarajia kufikia hapa. Tuliamini kila mara kuwa tuna uwezo, lakini hatukuwa tunapata matokeo mazuri.

Wakati huo huo waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na kansela wa Ujerumani Angela Merkel watasitisha kwa muda majadiliano yanayohusiana na vita pamoja na mizozo ya kiuchumi duniani katika mkutano wa mataifa yenye utajiri mkubwa wa viwanda duniani G8 leo na kutazama burudani ya fainali ya kombe la Champions League kwa pamoja kati ya Chelsea na Bayern Munich wakiwa Camp David nchini Marekani.

Barcelona's coach Josep Guardiola is seen during the match against Chelsea during a Champions League semifinal second leg match at the Camp Nou stadium in Barcelona, Spain, Tuesday, April 24, 2012. Chelsea drew 2-2 with Barcelona to win the match 3-2 on aggregate. (Foto:Emilio Morenatti/AP/dapd)
Josep Pep Guardiola anasakwa na FC Liverpool kuinoa timu hiyoPicha: AP

Wakati tukisubiri matokeo kati ya Chelsea na Bayern Munich katika fainali ya kombe la Champions League, Liverpool ya Uingereza imo mbioni kumsaka kocha mpya baada ya uongozi wa timu hiyo kumpa kisogo kocha wake wa msimu huu Kenny Dalglish. Katika orodha ya makocha 11 hadi sasa wanaofikiriwa huenda wakazungumza na uongozi wa Liverpool, yamo majina ya makocha Pep Guadiola aliyeitupa mkono FC Barcelona msimu huu , kocha wa Wigan Athletics Roberto Martinez ambaye ameruhusiwa tayari na uongozi wa klabu yake kuzungumza na Liverpool, Brendan Rodgers wa Swansea ambaye tayari amepiga stop mazungumzo ya aina yoyote, Didier Deschamps wa Marseille, Frank de Boer wa Ajax , Paul Lambert wa Norwich City na pia Jürgen Klopp wa mabingwa mara mbili wa Bundesliga Borussia Dortmund.

Wamiliki wa klabu hiyo kutoka Marekani Fenway Sports Group wamesema nafasi ni finyu ya kumpata Pep Guadiola, lakini itakuwa si kumtendea haki iwapo hawatajaribu kutupa mshipi kwa kocha huyo nguli.

Kwa taarifa hiyo mpenzi msikilizaji ndio sina budi kusema tumefikia mwisho wa kuwaletea habari hizi za michezo kutoka DW mjini Bonn. Jina langu ni sekione Kitojo, hadi mara nyingine kwaherini.

Mwandishi: Sekione Kitojo/rtre/afpe/dpae

Mhariri: Josephat Charo