1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich kidedea dhidi ya Dortmund

Sekione Kitojo
7 Agosti 2017

Bayern Munich  yanyakua  taji  la  kwanza  la  msimu , Super Cup dhidi  ya  mahasimu  wao  wakubwa  Borussia Dortmund ligi kuanza tarehe 18 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/2hpxm
DFL Supercup 2017 - Borussia Dortmund  vs Bayern Muenchen
Baadhi ya wachezaji wa Bayern wakishangiria ushindi katika Super Cup mjini DortmundPicha: Getty Images/Bongarts/A. Grimm

Bayern Munich  siku  ya  Jumamosi ilitoka  kidedea  katika uwanja  wa  Signal Iduna Park  mjini  Dortmund  baada  ya kuishinda  Bourissia Dortmund  kwa  mabao 7-6  kwa  njia ya mikwaju  ya  penalti  baada ya  timu  hizo vigogo  katika ligi  ya  Ujerumani  Bundesliga  kutoshana  nguvu  katika dakika 90 za  kawaida  kwa  kufungana  mabao 2-2.  Hata hivyo  kulikuwa  na  kwikwi  katika  mchezo  huo  kutokana na  kushindwa  kufanyakazi  mfumo  wa  kutambua  mabao kwa  njia  ya  vidio  ikiwa  ni jaribio  la  kwanza  kubwa kabla  ya   kutumika  mfumo  huo  katika  ligi  ya Bundesliga.

Deutschland DFL-Supercup Dortmund gegen Bayern
Borussia Dortmund wakishangiria bao lao katika mchezo huo wa Super Cup uliotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Bayern Picha: Reuters/W. Rattay

Chama  cha  kandanda  nchini  Ujerumani DFB na  chama kinachoendesha  ligi  hiyo DFL, vimesema  katika  taarifa ya  pamoja  kwamba  mfumo  huo wa  kuwasaidia  waamuzi kwa  njia ya  video  ulishindwa  kufanyakazi katika  mchezo huo  wa  Jumamosi  nyumbani  kwa  Borussia  Dortmund, na  kuzusha  mjadala  juu teknolojia  hiyo  mpya.

Refa  alikuwa  ana  jaribu  kutambua  iwapo  Joshua Kimmich  wa  Bayern Munich  alikuwa  ameotea  wakati alipompatia  pasi Robert Lewandowski  na  kupachika  bao la  kusawazisha  bao  la  Dortmund  lililowekwa  kimiani  na Christian Pulisic katika  dakika  za  mwanzo.

Deutschland Fußball Bundesliga Bayern München - Borussia Dortmund
Mchezaji wa bayern Joshua KimmichPicha: picture-alliance/kolbert-press

Mistari ya  kuonesha  kwamba  mchezaji  ameotea  ama  la katika  video  haikuwapo  katika  sehemu  ya  kwanza  ya mchezo  huo  kutokana  na matatizo ya  kiufundi, wamesema  maafisa  wa  vyama  hivyo , ikiwa  na  maana refa  alilazimika  kutoa  uamuzi  bila ya  mfumo huo wa usaidizi.

Ligi  ya  Ujerumani inaanza  rasmi  tarehe  18  mwezi  huu, siku  ya  Ijumaa  kwa  mchezo  kati  ya  mabingwa  watetezi Bayern  Munich  dhidi  ya  Bayer  Leverkusen.

Deutschland Bayer Leverkusen | Lars und Sven Bender
Wachezaji wa Bayer Leverkusen Picha: imago/U. Kraft

Dortmund  inaanza  kampeni  ya  msimu  huu  ugenini dhidi  ya  Wolfsburg , siku  moja  baada  ya  ufunguzi  wa msimu , na  wanakabiliwa  na  mwanzo mgumu  kwa kupambana  na  Hertha Berlin , kisha  Freiburg na FC Kolon , timu  zote  zikiwa  katika  timu  saba  bora  za  ligi msimu  uliopita.

 

Mwandishi: Sekione Kitojo/dpae,afpe,rtre,ape

Mhariri: Mohammed Khelef