1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich kidedea, Marco Reus arejea uwanjani

Sekione Kitojo
12 Februari 2018

Bayern hadithi ni ile ile, inaendelea kuongoza ligi ya Ujerumani Bundesliga, na timu zinazoifuatia zinasua sua,  Marco Reus wa Borussia  Dortmund arejea uwanjani baada ya karibu mienzi minane akiwa  majeruhi.

https://p.dw.com/p/2sXyk
Deutschland FC Bayern München v FC Schalke 04 - Bundesliga
Picha: imago/IMAGEPOWER/M. Weber

Bayern Munich imeendelea  kuonesha  ubabe  wake katika  ligi  ya Ujerumani  Bundesliga, ambapo Jumamosi  hii  iliizaba  Schalke 04 kwa  mabao 2-1  ikiwa  nyumbani, wakati  ambapo kocha  wake mkuu  Jupp Heynckey  hakuwapo  uwanjani  kuiongoza  timu  hiyo kutokana  na  kuugua  homa.

Deutschland FC Bayern München v FC Schalke 04 - Bundesliga
Wachezaji wa Bayern Munich wakimaliza mchezo dhidi ya Schalke kwa ushindiPicha: picture alliance/abaca/A. Gebert

Bayern  inaongoza  kwa  pointi 18 , ikifuatiwa  na RB Leipzig ambayo  wiki  iliyopita  ilikuwa  katika  nafasi  ya  tatu, na  nafasi hiyo  ya  pili  ikishikiliwa  na  Bayer Leverkusen.

Lakini  baada  ya  Bayer Leverkusen  kushinda  katikati  ya  wiki katika  mchezo  wa  kombe  la  shirikisho  nchini  Ujerumani DFB Pokal dhidi  ya  Werder  Bremen, kwa  mabao 4-2, ushindi  huo uliigharimu  timu  hiyo kwa  kuwa  wachezaji  walionekana  kuwa  na miguu  mizito na  kukubali  kipigo  cha  mabao 2-0  nyumbani  dhidi ya  Hertha  BSC  Berlin. Akielezea  kuhusu mbinu za  mchezo  huo zilivyopangwa na  kocha  mkuu  wa  Hertha Berlin Pal Dardai , mchezaji  wa  kati  wa  Hertha Valentino Lazaro aliyefunga  bao muhimu la pili  katika  mchezo  huo alisema.

"Kazi  yangu  leo ilikuwa kukaa kwa  muda  mfupi sana  na  mpira, badala  yake kucheza kwa pamoja zaidi na kufanya haraka kuelekea katika  lango  la  adui. Kulia sikuwa napata mipira ya mara nyingi, kwa hiyo nikabadilisha  upande, kwa  kuwa  nilikuwa  na  hisia kwamba  adui ametambua mbinu  hiyo. bila  shaka  baada  ya kushika mpira  wa kwanza  ama  wa  pili kila  kitu  kilikuwa sahihi. Nimefurahi  sana jinsi mambo  yalivyokwenda na  nafarijika kuhusu pointi tatu leo."

Bundesliga | Bayer Leverkusen vs Hertha BSC
Pambano kati ya Bayer Leverkusen dhidi ya Hertha BerlinPicha: Reuters/T. Schmuelgen

Kwa  mara  ya kwanza katika mwaka  huu  wa  2018 , Borussia Dortmund imeweza  kupata  pointi  zote  tatu katika  uwanja  wake wa  nyumbani , baada  ya  kutoka  sare  mara  mbili.

Marco Reus arejea uwanjani

Lakini  habari hizo nzuri  kwa  mashabiki wa  Borussia  Dortmund  ziliongezewa hamasa baada  ya  kuonekana  kwa  mara  ya  kwanza  mshambuliaji mashuhuri  wa  timu  hiyo Marco Reus ambaye  alikuwa  nje  tangu aliposhiriki  katika  mchezo  wa  fainali  ya  kombe  la  shirikisho nchini  Ujerumani DFB Pokal mjini  Berlin  ambapo Borussia  iliibuka mshindi  kwa  kuishinda Eintracht Frankfurt  kwa  mabao 2-1  mwezi wa May  mwaka  jana na  kujikuta  nje  ya  uwanja  kwa  kuwa majeruhi kwa  muda  mrefu.

Marco  alionesha  kwamba anahitajika sana  katika  kikosi  hicho  cha  kocha  Peter Stoeger ambacho kiishinda  Hamburg SV kwa  mabao 2-0  nyumbani. Huyu  hapa Marco Reus.

Deutschland Marco Reus
Marco Reus (katikati) akikabiliwa na wachezaji wa Hamburg SVPicha: imago/M. Müller

"Hata  mimi  nimefurahi  sana. Ni faraja  kubwa  kushiriki  tena uwanjani. Nilifanyakazi kwa juhudi  kubwa  sana, ili  niweze kurejea uwanjani. Hatukuonesha mchezo   mzuri  sana , lakini  katika  hali halisi, sijali  sana, lakini  pointi  ni  muhimu  sana kwa  sasa , ili tuweze kubakia  katika  nafasi  za  juu. Hamburg walitubana  sana leo na  kufanya  kazi  kuwa  ngumu kwetu. Haikuwa bure  kwamba walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Leipzig wiki  iliyopita."

Borussia  Dortmund imesogea hadi  nafasi  ya  tatu  ikiwa  na  pointi 37, ikifuatiwa  na  Eintracht  Frankfurt  ambayo  ina  pointi 36, Bayer Leverkusen  imeshuka  kutoka  nafasi  ya  pili  wiki  iliyopita  hadi nafasi  ya  5 ikiwa na  pointi 35, ikifuatiwa  na  Schalke 04  na FC Augsburg  katika  nafasi  ya  6 na  TSG Hoffenheim baada  ya kupata  ushindi  mnono wa  kwanza  katika  mwaka huu  wa  2018 wa mabao 4-2 dhidi  ya  Mainz 05 imetua  katika  nafasi  ya 8. Huyu hapa  kocha  wa  TSG Hoffenheim Julian Nagelsmann.

Deutschland Bundesliga: Hoffenheim - Mainz 05 | Andrej Kramaric
Mshambuliaji wa TSG Hoffenheim Andrej Kramric (kulia)akishangiria baoPicha: picture alliance/dpa/U. Anspach

"Katika  siku  za  nyuma kila  mara  tulikuwa  tunapata upungufu, kwamba  tunapata mabao machache kutokana  na  nafasi tunazopata na  juhudi  zetu tunazoweka. Na  leo tulifunga  kambi  katika  eneo  la adui, tukipata mipira mingi inayorudishwa na walinzi wa timu pinzani na ndipo  bao  la  kwanza  la Andre lilivyopatikana. Wiki  mbili zilizopita , nafikiri, hatungeweza  kulazimisha  mpira uingie wavuni. Lakini  leo tumeweza, na  nimefurahi  sana kwa  hilo."

Lakini  hata  hivyo  pambano  la  kuvutia  zaidi  lilikuwa  kati  ya  timu mbili zilizoko  katika  nafasi  ya  kushuka  daraja. Werder Bremen katika  nafasi  ya  16 ilijitutumua  na  kutoka kifua  mbele  kwa kuizaba Wolfsburg  kwa  mabao 3-1, ikiikaribia  timu  hiyo  iliyoko katika  nafasi  ya  13 sasa kwa  tofauti  ya  bao moja.

Bundesliga | Eintracht Frankfurt - 1.FC Köln
Wachezaji wa FC Kolon wenye jezi nyekundu wakipambana na Eintracht FrankfurtPicha: imago/J. Huebner

Werder Bremen  imetoka  kutoka  nafasi  ya  16  sasa  iko  katika  nafasi  ya 15 pointi tatu juu  ya  Mainz 05  iliyoporomoka  hadi  nafasi  ya  16. FC Kolon  baada  ya  kichapo  cha  mabao 4-2  dhidi  ya  Eintracht Frankfurt imejichimbia  bado mkiani  mwa  ligi  ikiwa na  pointi 13, ikifuatiwa  na  Hamburg SV ambayo  nayo ina  pointi 17 timu  hizo zikipishana  kwa  pointi  4.

 

Mwandishi:   Sekione  Kitojo / dpae / afpe / rtre

Mhariri: Mohammed Khelef