1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich kuipiku Hoffenheim ?

28 Novemba 2008

Katika changamoto za Bundesliga :Munich wanacheza leo na Leverkusen.Hoffenheim na Bielefeld.

https://p.dw.com/p/G4UB
Luca Toni atamba hapo.Picha: AP

Kufuatia changamoto za champions League -kombe la klabu bingwa barani ulaya na kombe la UEFA kati ya wiki,timu mbali mbali zinarudi uwanjani leo na kesho kutamba katika Ligi:Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich, ambao walikata tiketi yao ya duru ijayo ya kutoana ya Champions League baada ya kuizaba Steua Bucharest ya Rumania mabao 3:0,wana miadi jioni hii na Bayer Leverkusen,waliopo nafasi ya pili katika ngazi ya Ligi-nyuma ya Hoffenheim.Katika medani ya riadha bingwa wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon,mzee Haile Gebrselassie anakimbia kesho katika mbio za marathon za Australia,akitumai kuivunja rekodi yake.

Bayern Munich katika changamoto yake hii leo na Bayer Leverkusen kileleni mwa Bundesliga, ndio yenye kushika mpini na itakua juu ya Leverkusen kuhimili vishindo vya akina Luca Toni,Miroslav Klose na Franck Ribbery-majogoo 3 waliowika majuzi katika champions League na mwishoni mwa wiki iliopita walipoikomea Energie Cottbus mbao 4-1 katika Bundesliga.

Leverkusen lakini, wanarudi leo uwanjani baada ya msukosuko wa mwishoni mwa juma lililopita walipozabwa mabao 2-1 na timu iliopo mkiani ya Armenia Bielefeld.Isitoshe, rekodi ya Leverkusen mbele ya mabingwa Munich haivuti.Mara ya mwisho kuilaza Munich ilikua msimu wa 2004 na hicho ni kitambo kirefu katika dimba.

Tangu Munich hata Leverkusen kila moja ina pointi 28-pointi 3 nyuma ya viongozi Hoffenheim.Munich inayotaka kwenda likizo ya X-masi na mwaka mpya ikiwa mabingwa wa nusu-msimu ,wana miadi na Hoffenheim mwishoni mwa wiki ijayo kuamua nani kati yao ataparamia kileleni.

Hoffenheim baada ya kuizaba Cologne 3-1 jumamosi iliopita,iko nyumbani leo kutamba tena mara hii mbele ya Bielefeld.

Stuttgart ilimtimua kocha wake aliewatawaza mabingwa 2007 Armin Veh na chini ya kocha mpya Markus Babbel, wana miadi kesho jumapili na Schalke.Hawatakua na kazi rahisi. Kesho pia Hamburg inalenga ushindi tu mbele ya Bochum baada ya kuibomoa Bremen wiki iliopita kwa mabao 2:1.Duru ya mwishoni mwa wiki hii ya Bundesliga-ilifunguliwa ijumaa kwa mpambano kati ya Berlin na FC Cologne.

Mapambano mengine ni kati ya Bremen na Frankfurt,Hannover na Karlsruhe,Borussia Monchengladbach na Cottbus .Borussia Dortmund na Wolfsburg zitakamilisha kalenda ya mapambano hapo kesho.

Katika changamoto za Premier League,Ligi ya Uingereza, kinyanganyiro kinaendelea kileleni kati ya Chelsea na Liverpool. Liverpool iinaingia uwanjani mwishoni mwa wiki hii ikiwa imepata pigo la kuumia kwa stadi wake Fernando Torres.

Torres atakua nje ya chaki ya uwanja kwa muda wa wiki mbili baada ya kuumia katika mpambano wa champions league, juzi jumatano Liverpool ilipocheza na Marseille.Stadi huyo wa timu ya taifa ya Spian,mabingwa wa Ulaya, alirudi karibuni tu uwanjani kufuatia kuumia kwake na kuwa nje ya uwanja kwa wiki 5.Mlinzi wa Liverpool Fabio Aurelio pia ameumia na hatacheza kwa muda wa wiki mbili.

Chelsea ina miadi kesho na Arsenal na stadi wake kutoka Ivory Coast, Didier Drogba aliekuwa pia nje ya uwanja kwa kuumia na halafu akafungiwa kucheza kwa kuwarushia peni mashabiki waliomrushia Chelsea ilipolazwa na Burnley katika League Cup,amesema miezi ya karibuni ndio ya misukosuko mingi kwake.Lakini alisema aliwahi kujikuta katika misukosuko mikubwa kama hiyo na anaamini atavuka pia salama na misukosuko ya sasa. Kesho ni Manchester United inachuana na Manchester City.

Kuhudhuria kwa mashabiki uwanjani kumepungua kwa kima cha wastani cha mashabiki 920 kwa kila mechi-hii ni kwa muujibu ya uchunguzi uliofanywa na gazeti la Daily Telegraph la Uingereza.

Katika medani ya riadha: kesho ni zamu ya mbio za kwanza mashuhuri za marathon nchini Australia-Great Australian Run.Badala ya km 42 lakini, mara hii ni km 15.

Bingwa wa marathon wa dunia-Gebrselassie,akiwa na umri wa miaka 35 ni mwanariadha pekee aliekimbia mbio kamili za marathon chini ya masaa 2 na dakika 4.Ilikua Berlin,Septemba,mwaka huu alipoiweka rekodi ya dunia katika muda wa masaa 2:03.59. Kesho Gebre haahidi mengi,kwani ni mbio zake za kwanza tangu Berlin.