1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern munich na Hertha Berlin kileleni mwa Bundesliga

Ramadhan ali20 Agosti 2007

Katika kombe la klabu bingwa barani afrika Al Hilal ya Sudan yaizaba Al Ahly ya Misri mabao 3:0

https://p.dw.com/p/CHbF

Katika Bundesliga, Hamburg iliizaba jana Bayer Leverkusen na kuparamia kileleni mwa Bundesliga pamoja na Bayern Munich .Mkwaju wa adhabu wa penalty aliouchapa nahodha wao Rafael van der vaart anaetapia kuhamia Valencia,Spain, ulitosha kuwachimbia kaburi Bayer Leverkusen na kuwapokonya jana pointi 3.

Bayern munich tayari jumamosi iliirarua mapande mawili Werder Bremen na kuwazaba mabao 4:0.

Bremen haikuwa na jibu la hujuma za akina Ribery,Luca toni na Miroslav Klose.

Klose alitiwa munda na Ronaldo-mlinzi wa Bremen kutoka Brazil na anachechemea .ni vigumu sasa iwapo ataongoza hujuma za Ujerumani keshokutwa jumatano pale Ujerumani itakapoumana na Uingereza uwanjani Wembley.

Kuhusu ngware aliochezewa na Ronaldo,Klose alisema:

“Ni maumivu makubwa niliopata.sikuweza kuona kwenye kamera ya picha ya marudio jinsi ilivyotokea ,lakini nimehisi kuwa alinitimba mguuni juu na chini.Lakini najua siwezi kumlaaumu Ronaldo,naelewa akiulenga mpira na ninamuelewa vya kutosha mchezo wake.”

Alisema Miroslav klose, aliekodolewa macho jumamosi uwanjani kwani hadi karibuni akiichezea werder Bremen katika uwanja huo.

Nae kocha wa Bremen Thomas Schaaf alisema:

“Baada ya kukandikwa mabao 2:0 ,hatukuwa tena jibu”.

Asema kocha Schaaf.Mabingwa Stuttgart wameangukia nafasi ya 15 ya ngazi ya Ligi ,kwani wana pointi 1 tu katika mapambano 2.Walizabwa mabao 3-1 na Hertha Berlin hapo jumamosi.

Katika Premier League-ligi ya Uingereza, mabingwa Manchester united , wamelazwa na Manchester City,chini ya kocha mpya Sven-Goran Eriksson,-kocha wa zamani wa Uingereza bao 1:0.

Huu ni ushindi 3 wa Manchester city inayoongoza kilelelni kwa pointi 2.Hii ni mara ya kwanza kwa Manchester united tangu kupita miaka 15 kuanza vibaya katika Ligi ya Uingereza.

Chelsea inayofuata nyuma ya Manchester city, ilimudu suluhu ya bao 1:1 na FC Liverpool.Arsenal imetoka nayo sare bao 1:1 na Blackburn Rovers.

Al Hilal ya sudan imewaadhibu vikali kabisa mabingwa wa afrika Al Ahly ya Misri walipoichapa mabao 3:0 uwanjani oumduraman na kuwarejesha Cairo kikapu kitupu.Mabao ya Dario Khan na Hassan Ashag mnamo muda wa dakika 10 tu za kipindi cha pili yalitosha kwa Al Hilal kutamba mbele ya mabingwa wa Afrika na kuparamia wao killeni mwa kundi lao.

Ingawa kila moja ina pointi 9,Al hilal inaongoza sasa kwa magoli.Hilio ni pigo la pili kwa Al Ahly baada ya lile walilopata kutoka kwa Esperence ya Tunisia la bao 1:0.

ASEC Abidjan ya Ivory Coast wako pointi 2 nyuma ya timu hizo 2 .Waliizaba Esperence mabao 2:0 katika kipindi cha pili cha mchezo.

Ama katika changamoto ya kombe la shirikisho-Confederation Cup, mshambulizi wa TP Mazembe Tresor Mputu alilifumania dakika za mwisho lango la CS Sfaxien ya Tunisia katika ushindi wa mabao 2-1 wa wakongomani.Ushindi huo umeinyanyua juu TP mazembe na kuipiku Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ingawa kwa magoli.

Kocha wa Black Stars-Ghana-Claude Le Roy amepanga kuutumia mpambano kati ya Ghana na Senegal kesho mjini London, kuwajaribu chipukizi anaotumai kutamba siku zijazo.Amemuita Dede Ayew kutoka Olympique Marseille,Mario Barwuah kutoka Inter Milan na Yahaya Mohammed kutoka Nice.

Ayew ni motto wa nahodha wao wa zamani Abedi Ayew Pele.

Senegal nayo kwa upande wake imeamua kutojaribu chipukizi bali kumuita mkongwe El Hadji Diouf kujiunga na kikosi chao cha wachezaji 20 kwa changamoto ya kesho mjini London na Black Stars-Ghana.Senegal inajinoa kwa mpambano na Burkina faso kuania tiketi ya kombe lijalo la Afrika nchini Ghana.

Kombe la chipukizi la CECAFA chini ya umri wa miaka 17 linaendelea huko Bujumbura huku jumla ya timu 7 zikiania taji hilo:Katika kundi A kuna Ruanda,Tanzania-bara,Somalia na Burundi wenyeji wakati kundi B: Lajumuisha Uganda,Kenya na Zanzibar iliomudu suluhu na Somalia ya bao 1:1.

Mwanamichezo wetu Bakari Ubena asimulia kutoka Bujumbura:

Mashindano ya ubingwa wa riadha ya dunia yataanza mwishoni mwa wiki hii huko Osaka,Japan huku mataifa 203 yakishiriki na hii ni rekodi.IAAF-shirikisho la riadha ulimwenguni ambalo rais wake Lamine Diack kutoka Senegal anagombea tena wadhifa huo keshokutwa,limetaja idadi ya nchi zinazoshiriki yavunja rekodi ya 1999 iliowekwa huko Seville,Spain.Ni nchi 9 tu kati ya wanachama wote 212 wa IAAF hawashiriki.

Kikosi cha Tanzania cha wanariadha 6,kiliondoka leo kuelekea Osaka,Japan.