1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern Munich yatawazwa Bingwa wa Ujerumani

10 Mei 2010

Chelsea bingwa wa Uingereza

https://p.dw.com/p/NKen
Bayern Munich na taji lao 22.Picha: AP

Bayern Munich, yatwaa taji lake la 22 la Bundesliga na inajinoa sasa kwa finali ya Kombe la klabu bingwa barani ulaya-Champions league kati yake na Inter Milan ya Itali.

Chelsea,yatoroka na taji la Premier League huku Manchester United, ikiahidi msimu ujao itarudi kutamba hata zaidi.

Katika Kombe la Shirikisho la Afrika, mabingwa wa Tanzania-Simba hawakunguruma huko Alexandria walibnebshwa mabao 5-1 na Wamisri Harras al-Hadoud.

Mtanzania Mohamed Msenduki Ikoki na muethiopia Almaz Alemu washinda mbio za marathon za Mainz wakati katika Prague-marathon ,mkenya Eliud Kiptanui akiikosea kidogo tu kuifuta rekodi ya Muethiopia,Haile Gebreselassie.

Kama ilivyotarajiwa Bayern Munich,imevishwa taji lake la 22 msimu huu hapo Jumamosi, baada ya kuizamisha daraja ya pili Hertha Berlin kwa mabao 3:1.

Kwa ushindi huo,Munich ilimaliza msimu katika Uwanja wa olimpik wa Berlin ikiwa na pointi 5 zaidi kuliko Schalke,ilioibuka makamo-bingwa.Munich ikawa pointi 9 mbele ya Werder Bremen iliomaliza nafasi ya 3.Ni Timu hizo 2 au 3 zinazoweza msimu ujao kuiwakilisha Bundesliga katika Champions League-kombe la klabu bingwa barani ulaya.

Munich ilikuwa na sherehe maalumu jana katika ukumbi wa jiji la Munich,mbele ya maalfu ya mashabiki wake.kikosi kizima cha kocha Louis van Gaal, kilijitembeza katika roshani ya Jumba hilo la manispaa:

Baadae , kocha van Gaal akanadai:

"Sisi ndio timbu bora kabisa Ujerumani na pengine ulaya nzima."

Hapo van Gaal ,akiashiria uwezekano wa Bayern Munich, kutawazwa Mei 22 ,mwaka huu , mabingwa wa Ulaya, mjini Madrid,Spain , endapo wakiilaza Inter Milan katika finali ya Champions league. Ijumamosi ijayo, Bayern Munich, itarudi Uwanja wa Olimpik wa Berlin, ilikovishwa taji la Bundesliga juzi kwa finali ya Kombe la Taifa-Kombe la Shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB) kupambana na Werder Bremen . Munich , inalenga kuvaa mataji 3 msimu huu-mawili nyumbani na 1 ulaya.

Taji la mtiaji mabao mengi katika Bundesliga, lilikwenda kwa Mbosnia Edin Dzeko, wa klabu bingwa msimu uliopita,Wolfsburg. Edin, alipachika mabao 22 akimpiku mshambulizi wa Bayer Leverkusen,Stefan Kiessling alietia mabao 21.Lucas Barrios wa B. Dortmund, alifuata nafasi ya 3 kwa mabao 19 huku Kevin Kuranyi,wa Schalke 04-makamo-bingwa, akiondokea nafasi ya 4 kwa mabao 14.

Klabu 2 zinashuka daraja ya pili kutoka ya kwanza:Mbali na Hertha Berlin-klabu ya jiji kuu,Bochum ni klabu ya pili baada ya kuzabwa mabao 3:0 na Hannover iliokumbwa na msiba mkuu msimu huu kwa kujiua kipa wao na wa Taifa: Robert Enke. Nüremberg ina nafasi ya kujiokoa kwa kucheza mpambano maalumu kati yake na Augsburg.

Ama katika Premier League-ligi ya Uingereza, Chelsea, ikiongozwa na kocha mtaliana, Carlo Ancelotti, imeipiku tena Manchester United na kutoroka na taji la Premier League. Kocha Ancelott, amempelekea salamu kocha wa Manu, Sir Alex Ferguson, kwamba Chelsea, ina azma ya kutawala dimba la Uingereza kwa miaka mingi ijayo .Hii ni baada ya Muivory Coast, Didier Drogba na wenzake kutoroka jana na taji la Premier League msimu wake wa kwanza tu mtaliana huyo.Chelsea, ilimaliza msimu kwa kishindo ilpipoizaba jana Wigan Athletics mabao 8:0 na kuipiku Manchester United kwa pointi 1.

Jibu la kocha wa Manu ,Sir Alex Ferguson, ni kuwa timu yake, itarudi uwanjani msimu ujao ikiwa kali zaidi kuliko msimu huu.Kwa mara ya kwanza tangu kupita miaka 4, kikosi cha Sir Alex, hakikufua dafu.Hii inafuatia pigo walilopata Champions League walipopigwa kumbo nje ya nusu-finali na Bayern Munich. Sir Alex hatahivyo, aliipongeza Chelsea, jinsi ilivyotamba msimu huu na akasema timu ya Ancelotti,ilistahiki ushindi wake.

Ama katika La Liga,Ligi ya Spain, FC Barcelona, ikitamba na Lionel Messi, iko nayo njiani kutetea taji lake baada ya kutolewa jasho na wachezaji 10 tu wa Sevilla na kuondoka na ushindi wa mabao 3:2.Mabao ya Sevilla, yalitiwa na stadi wa Mali Frederi Kanoute na Mbrazil, Luis Fabiano.

Real Madrid nayo ilitia kasi kuifukuzia Barcelona, kileleni na kuweka mlango wazi wa kuwatia munda wasitoroke na Kombe. Mpambano 1 ukisalia kabla ya Barca kuvaa taji na wakiongoza kwa pointi 1 tu, Real ilivuma kwa kishindo ilipoizaba Athletico Bilbao mabao 5-1.

Katika kinyan'ganyiro cha Kombe la Shirikisho la dimba la Afrika-Confederations Cup, Enyimba ya Nigeria, ilimaliza vita vyake na Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kwa ushindi wa mabao 3-0 na hivyo Enyimba, imeitimua nje Vita kwa mabao 9-8 kufuatia changamoto za mikwaju ya adhabu ya penalty. Timu hizo 2 zilijikuta sare 3:3 kufuatia duru zao mbili. Mjini Harare, CAPS United ya Zimbabwe, ilitamba mbele ya Wariri Wolves ya Nigeria.

Mvua ya magoli iliwanyeshea Simba wa Tanzania huko Alexandria,Misri.Simba wakiroa maji chapa-chapa, wanarudishwa keshokutwa nyumbani Dar-es-salaam, kikapu tele kikijaa mabao 5:1 kama mwanamichezo wetu George Njongopa anavyosimulia kutoka Dar-es-salaam.

Mjini Mombasa, ilikua zamu tena ya mbio za nyika na madume wa nyumbani Kenya, tena walitamba tena.Lakini Eric Ponda ,kwanza anatuchukua katika Ligi ya Kenya,ingawa mwishoni mwa wiki mabingwa Sofapaka,hawakuwa uwanjani:

Tukibakia katika medani ya riadha,mabingwa wa marathon wa Kenya na Tanzania walitamba pia huku ulaya: Wakati katika Prague-marathon huko Jamhuri ya Czech,mkenya, Eluid Kiptanui, alishinda kwa muda maridadi wa masaa 2:05:39 akifuatwa nafasi ya pili na Muethiopia ,Yemane Tsegey.Nicholas Kipruto Koech,alibidi kuridhika na nafasi ya 3 hapo.

Ama mjini Mainz,Ujerumani ,ushindi wa Mainz -marathon ,ulikwenda kwa mtanzania Mohamed Msenduki Ikoki kwa muda wake wa masaa 2:11:01. Upande wa wanawake, nafasi ya kwanza ilikwenda kwa Almaz Alemu.

Mwandishi: Ramadhan Ali/DPAE/AFPE/SID

Uhariri: Mtullya Abdu