1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yajiwinda kumnasa mlinda mlango wa Schalke

19 Aprili 2011

Mlinda mlango wa Ujerumani anayechezea Schalke 04 Manuel Neuer inaarifiwa kuwa anajiandaa kutia saini mkataba wa miaka minne kuichezea Bayern Munich.

https://p.dw.com/p/10wdt
Manuel NeuerPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la kila siku hapa nchini the Bild limearifu kuwa Bayern inapanga kumnunua mlinda huyo kwa kitita cha Euro millioni 20.Neuer mkataba wake kuidakia Schalke unamalizika mwakani.

Wakati Schalke ikijiwinda kupambana na Manchester United katika nusufainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, pia timu hiyo inapambana kumbakisha Neuer.

Neuer mwenyewe hapo siku ya Jumamosi alisema kuwa uamuzi wa wapi atakwenda, tayari umekwishafanywa, lakini hata hivyo hakufichua ni wapi.

Mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich Christian Nerlinger amedokeza kuwa Neuer msimu ujayo atakuwa katika milingoti mitatu ya timu hiyo.

Baada ya ushindi wa mabao 5-1 iliyoupata Bayern Munich hapo siku ya Jumapili dhidi ya Bayer Leverkusen katika mechi za Bundesliga, Nerlinger aliweka wazi kuwa majogoo hao wa soka nchini Ujerumani wanajiwinda kupata saini Manuel Neuer.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Schalke Clemens Toennies alisema kuwa watafanya kila liwezekenalo kumbakisha mlinda mlango huyo ambaye amemuelezea kuwa ni kioo na sura ya Schalke.

Bayern Munich imekuwa ikihangaika kutafuta mtu atakayekuwa imara zaidi mlangoni tokea nahodha wa zamani wa Ujerumani Oliver Kahn alipostaafu

Wakati huo huo timu ya FC Cologne Jumanne imetangaza kuwa kocha wake Frank Schaefer ataachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu.Klabu hiyo inayoshiriki katika Bundesliga ambapo inakamata nafasi ya 12, imesema sababu za kuondoka kwa kocha huyo ni za kibinafsi.

Schaefer ambaye alichukua jukumu ya ukocha wa FC Cologne Oktoba mwaka jana kutoka kwa Zonimir Soldo aliyetimuliwa amesema anategemea tangazo lake hilo halitowaathiri wachezaji na kwamba wataelekeza akili zao katika mechi zilizosalia za ligi hiyo ya Bundesliga.

Ijapokuwa timu hiyo inakamata nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi, lakini bado haina uhakika wa kutoshuka daraja kwani iko pointi sita juu ya mstari wa kushuka d araja.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/AFP/DPA

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman