1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern kukutana na Stuttgart

Admin.WagnerD6 Novemba 2015

Mabao yanatarajiwa kufungwa kwa fujo leo Jumamosi katika ligi ya kandanda hapa Ujerumani - Bundesliga wakati safu kali kabisa ya mashambulizi ikikutana na safu dhaifu kabisa ya ulinzi.

https://p.dw.com/p/1H1Mr
Fußball Bundesliga 3. Spieltag FC Bayern München vs. VfB Stuttgart
Picha: REUTERS/M. Dalder

Vijana wa Pep Guardiola wako kileleni na tofauti ya pointi tano na ndiyo timu pekee hapa Ujerumani ambayo haijashindwa mchuano wowote katika 11 za mwisho wakati Stuttgart wakiwa katika eneo hatari la kushushwa daraja.

Bayern ina washamuliaji hatari sana na hadi sasa Thomas Müller na Robert Lewandowski wamefunga kwa pamoja magoli 31 katika mashindano yote yakiwemo mabao 23 katika Bundesliga.

Kinyume chake ni kuwa safu ya ulinzi ya Stuttgart imemeza magoli 23 kufikia sasa, ikiwa ni rekodi mbaya kabisa katika Bundesliga pamoja na washika mkia Augsburg. Stuttgart wamepoteza mechi zao 13 za mwisho dhidi ya Bayern katika mashindano yote. Mchuano muhimu wa wikendi hii hata hivyo ni hapo kesho kati ya nambari mbili Borussia Dortmund dhidi ya nambari nne Schalke katika debi ya Bonde la Ruhr.

Borussia iliwazaba watani wao tatu bila mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika uwanja wa Dortmund wa Westfalenstadion mwezi Februari wakati wenyeji walipofyatua langoni makombora 31 ikilinganishwa na matatu tu ya Schalke.

Borussia Moenchengladabach watatafuta ushindi wao wa saba mfululizo katika Bundesliga chini ya kaimu kocha Andre Schubert wakati wakiwaalika Ingolstadt katika uga wa Borussia Park hii leo wakilenga kuweka historia ya Bundesliga.

Hakuna kocha aliyewahi kushinda mechi zake saba za kwanza katika Bundesliga – hata kocha wa Bayern Pep Guardiola alifaulu tu kushinda zake tatu za kwanza katika mwaka wa 2013.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Gakuba Daniel