1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yaonja kichapo

Bruce Amani
29 Septemba 2016

Bayern Munich ilipata kichapo chake cha kwanza chini ya kocha Carlo Ancelotti wakati ilizamishwa moja bila na Atletico Madrid katika Champions League

https://p.dw.com/p/2QiGD
Fußball Atletico Madrid gegen Bayern München UEFA Champions League
Picha: Picture-alliance/dpa/J. Martin

Yannick Carrasco aliifungia Atletico bao hilo la pekee dhidi ya Bayern katika marudio ya mchuano wa nusu fainali mwaka jana, ambayo Wahispania hao walishinda. Atletico, licha ya kukosa kufunga penalti katika dakika za mwisho mwisho kupitia kwa mchezaji Antoine Griezmann, sasa inaongoza Kundi D na pointi sita wakati Bayern iko nafasi ya pili na pointi tatu. Rostov na PSV Eindhoven zina pointi moja kila mmoja baada ya kutoka sare ya 2-2 nchini Urusi.

Katika mchuano mwingine, Barcelona ililazimika kutoka nyuma na kuishinda Borussia Moenchengladbach mabao mawili kwa moja. Thorgan Harzad aliifungia Gladbach katika kipindi cha kwanza kabla ya Arda Turan na Gerard Pique kuifungia Barca katika kipindi cha pili cha mechi hiyo ya Kundi C.

Barca wanaongoza kundi hilo na pointi sita wakati Manchester City waliotoka sare ya 2-2 na Celtic wakishikilia nafasi ya pili na pointi nne.

Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Arsenal iliichabanga Basel 2-0, Paris Saint-Germain ikashinda 3-1 dhidi ya Ludogorets Razgrad, Besiktas ikatoka sare ya 1-1 na Dynamo Kiev nayo Napoli ikaizidi nguvu Benfica kwa kuilaza mabao 4-2.

Mwandishi: Bruce Amani/DPA
Mhariri: Sekione Kitojo