1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yazidi kujikuna kichwa kabla ya kukutana na Schalke

24 Februari 2012

Baada ya kipigo cha kushtusha mikononi mwa Basel, Bayern Munich inahitaji kuwazaba mahasimu wao katika ligi Schalke 04 Jumapili ili kupoesha shinikizo na kupunguza mwanya kati yao na viongozi Borussia Dortmund.

https://p.dw.com/p/149Vn
Bayern ilifungwa goli moja kwa sifuri na FC Basel katika mechi ya ligi ya mabingwa
Bayern ilifungwa 1-0 na FC Basel katika mechi ya ligi ya mabingwaPicha: picture-alliance/dpa

Bayern wamepata ushindi mara tatu katika mechi zao saba zilizopita na wakateremka kutoka kileleni mwa ligi hadi nafasi ya tatu, huku nafasi zao za kuendelea katika ligi ya mabingwa Ulaya zikizidi kufifia. Kuwasili kwa Schalke 04 katika nafasi ya nne pointi moja nyuma ya Bayern , kutakuwa mtihani kwa ujasiri wa Bayern katika uwanja wao wa nyumbani Allianz Arena. Ziara ya Schalke itawaleta pamoja wachezaji wawili wanaoongoza katika ufungaji mabao kwenye ligi Mario Gomez wa Bayern na Klaas-Jan Huntelaar wa Schalke.

Na wakati Bayern wakisuasua, mabingwa watetezi Dortmund wanalenga kunyakua ushindi wao wa saba mfululizo nyumbani watakapokutana na Hannover keshoJumapili. Dortmund wamepigwa jeki na kutokana na habari za uwezekano wa kurejea nyota wao Mjapan Shinji Kagawa; siku kumi tu baada ya kupata jeraha katika kifundo cha miguu.

Katika mechi za leo Jumamosi, Cologne itachuana na Bayer Leverkusen, VfB Stuttgart itakuwa mwenyeji wa Freiburg, Mainz 05 itaikaribisha Kaiserslautern, VfL Wolfsburg itacheza dhidi ya Hoffenheim, Augsburg dhidi ya Hertha Berlin, nayo Werder Bremen itafunga kazi na Nuremberg

Arsenal na Chelsea matatani

Kule Uingereza, kinyang'anyiro cha taji la ligi kuu ya England kati ya Manchester United na Manchester City kitazidi kupamba moto huku macho yote yakielekezwa kwa masaibu yanayovisakama vilabu vya Arsenal na Chelsea. Man City watachuana na Blackburn Rovers Jumamosi nao Man United watasafiri nyumbani kwa Norwich saa 24 baadaye.

Arsenal walikula magoli 4-0 nyumbani kwa AC Milan
Arsenal walikula magoli 4-0 nyumbani kwa AC MilanPicha: AP

Arsenal ambao wanakumbwa na msururu wa matokeo duni watakuwa mwenyeji wa Tottenham Hotspurs uwanjani Emirates katika mchuano wa jiji la London. Wakati Wenger akikosa usingizi, mwenzake wa Chelsea Andre Villas Boas naye anajikuna kichwa huku nafasi yake katika klabu hiyo ikizidi kutiliwa shaka. Chelsea inaonekana kuzongwa na masaibu chungu nzima ya usimamizi na leo itakutana na Bolton.

Zambia kuwapumzisha wachezaji wake

Mabingwa wa soka barani Afrika Zambia hawataingia tena uwanjani hadi mwezi Juni baada ya timu hiyo kufutilia mbali mchezo wa kirafiki kati yake na Gabon. Badala yake timu hiyo imeamua kuwapumzisha wachezaji wake baada ya ushindi wao wa kombe la mataifa ya bara la Afrika lililokamilika mapema mwezi huu kule Guinea ya Ikweta na Gabon.

Zambia awali ilisema ilitaraji kurejea katika uwanja ambao kulishuhudiwa mikwaju ya penalti iliyoamua mshindi wa fainali kati yao na Cote d'Ivoire, kwa mchuano wa kirafiki ijayo, lakini sasa wameiweka kando mipango hiyo.

Nahodha wa timu ya Zambia Christopher Katongo
Nahodha wa Zambia Christopher KatongoPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji wa Shirikisho la Soka la Zambia Erick Mwanza amesema Zambia imepokea idadi kubwa ya maombi ya mechi za kirafiki baada ya ushindi wao wa kombe la mataifa ya Afrika, lakini wameikataa yote kwa wakati huu.

Mchuano wao ujao utakuwa wa kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2014 dhidi ya Sudan Juni 4.

Na katika riadha Bingwa mara tatu wa Olimpiki Mjamaica Usain Bolt atakosa kushiriki mashindano ya riadha ya msimu kwa mara ya pili Jumamosi ili aweze kuendelea kufanya mazoezi yake. Wakala wake Ricky Simms hata hivyo hakutoa maelezo kuhusu ni lini Bolt atazindua kile Mjamaica huyo anataraji kuwa kitakuwa msimu maalum wa Olimpiki ambapo anatalenga kuhifadhi mataji yake katika mbio za mita 100 na 200 kwenye mashindano ya London.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman Mohammed