1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bei ya petroli dala 100 kwa pipa

3 Januari 2008

Bei ya mafuta ya petroli imepanda na kufikia kipimo cha juu kabisa cha dala 100 kwa pipa.kiu cha nishati kimeongezeka.

https://p.dw.com/p/Cjud

Bei ya mafuta ya petroli imefika kima cha dala 100 kwa pipa.Kwa bei hiyo, kiwango cha juu hadi sasa kimepindukiwa.

Muandishi wetu mjini Washington,Rolf Wenkel anasimulia hali iliopelekea bei ya mafuta kufikia kima hicho.

Maelezo yake mnasimuliwa studioni na Ramadhan Ali:

Bw.Eugen Weinberg,ndie bingwa anaeshughulikia soko la mali ghafi katika Commerzbank.Kwake yeye kufikia kima cha dala 100 kwa pipa la mafuta ya petroli tena siku ya kwanza ya biashara ya mwaka mpya kwa upande mmoja inasangaza na kwa upande mwengine kwa muda mujao alikwishatazamia kuwa hivyo.

„Hii imenisangaza.Kwa jicho la hatari za ukuaji uchumi ambazo tulijionea wiki na miezi michache iliopita,bei ya mafuta ya hadi dala 100 kwa pipa haistahiki.Lakini, ukiangalia matokeo ya kisiasa katika sehemu mbali mbali za dunia na masilahi ya vikundi vinavyovumisha uvumi kwa manufaa ya kujipatia faida na wawekazi wa muda mrefu ujao,bei hii ya juu haisangazi.“

Bei za mafuta kitambo sasa zimekuwa zikipanda kutokana na mahitaji ya mafuta yanayoongezeka kila pembe ya dunia na hasa kwa kustawi uchumi nchini China .

Sababu nyengine ya kupanda mno bei ya mafuta ni taarifa za kufungwa kwa bandari kadhaa za Mexico kutokana na hali mbaya ya hewa ,lakini pia habari kwamba shirika linalosafirisha mafuta la OPEC kuwa tangu 2004 halikuwa linamudu kukidhi mahitaji ya mafuta kwa wateja.Isitoshe, kumekuwapo mvutano baina ya kambi ya nchji za magharibi na mtoaji mkubwa mafuta ya petrolo-Iran pamoja na machafuko nchini Irak,hujuma katika mabomba ya mafuta nchini Nigeria huko Port Hercourt.Hata nchini Algeria, mashambulio yalifanyika katika bomba la mafuta.

Sababu nyengine ya kupanda mno kwa bei ya petroli yamkini ni athari za mlango wa nyuma zinazotokana na msukosuko wa banki yanayotoa mikopo ya majumba nchini marekani.Watiaji-raslimali katika mabenki hayo wanatoa amana zao na kuzitia katika biashara nono ya uzalishaji mafuta.

Bw.Weinberg wa Comerzbank ya Ujerumani anasema:

„Ndio, inawezekana mali-ghafi kwa jumla na hasa mafuta na dhahabu kuwa ndio bandari za usalama kwa watiaji raslimali kusafiria.Na ni mali ghafi hizo zinazonunuliwa.Ndio maana bei ya mafuta nayo inazinufaisha nchi zitaoazo mafuta.“

Bingwa huyu wa Comerzbank hakupendelea kubashiri kiasi gani bei ya mafuta itakavyokua robo ya kwanza ya mwaka huu kufuatia kumalizika majira ya baridi katika nchi za magharibi au hata mwishoni mwa mwaka huu.Anasema lakini yaweza ikateremka pale hali ya uchumi nchini Marekani ikiimarika na mahitaji ya mafuta na nishati yakipungua.

Kwani, anasema Weinberg, Marekani ni mtumiaji mkubwa wa mafuta ulimwenguni ikitumia kiasi cha robo ya nishati hii duniani.ndio maana msukosuko wa kiuchumi ulioikumba Marekani hivi sasa umeacha moja kwa moja athari zake katika bei ya mafuta ya petroli.

Mbali na mahitaji wazi wazi ya matumizi ya petroli kuna pia wanaovumisha kupanda kwa mahitaji ya mafuta na uvumi wao usidharauliwe.Kwani, ni jambo linalo uzito kwavile, bei za mafuta huwekwa katika masoko ya hisa na katika masoko hayo mchango wa fedha za uvumi ni mkubwa zaidi kuliko ule wa m ahitaji hasa.