1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIJING: Merkel aitaka China iongeze juhudi kuzuia mabadiliko ya hali hewa

27 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBVL

Kansela wa Ujerumani, Bi Angela Merkel, leo ameitaka China iongeze juhudi kuzuia mabadiliko ya hali ya hewa.

Mwito huo umezusha mjadala mkubwa kwamba nchi za magharibi zimekuwa zikiichafua anga kwa kipindi kirefu kuliko nchi zinazochipuka kimaendeleo kama vile China.

Bi Merkel yumo nchini China kwa ziara ya pili kama kansela wa Ujerumani, miezi minne kabla kufanyika mkutano wa kimataifa wa mawaziri wa mazingira unaotarajiwa kufanyika mwezi Disemba mwaka huu nchini Bali.

Mkutano huo unalenga kuanzisha mazungumzo yanayonuia kurefusha mkataba wa Kyoto kabla mwaka wa 2012.

Leo kansela Merkel ameishawishi China iheshimu sheria za kimataifa za kibiashara na maendeleo wakati alipokutana rasmi na waziri mkuu wa China, Wen Jiabao katika juhudi za kutafuta njia za kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na China.

´Inawezekana kuendelea vizuri kiuchumi kwa pamoja katika ulimwengu unaoendelea kukua, iwapo sheria zitaheshimiwa.´

Bi Merkel amesisitiza kuwepo sheria kali kulinda haki miliki na kuhakikisha ubora wa bidhaa, maswala ambayo China inalaumiwa kwa kutoyazingatia.