1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Beirut. Kambi ya wakimbizi yazingirwa.

2 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBvi

Majeshi ya Lebanon yakiwa na kiasi cha vifaru 50 na silaha kali wamesogea na kujiweka katika maeneo kuzunguka kambi ya wakimbizi wa Kipalestina ya Nahr al-Bared karibu na mji wa Tripoli, ambako Waislamu wenye imani kali wamekuwa wamejificha kwa muda wa wiki mbili.

Watu walioshuhudia wanaripoti kuwa maeneo ya wapiganaji wamekuwa wakishambuliwa kwa makombora katika kambi hiyo.

Majeshi ya usalama yanasema kuwa kiasi cha watu 19 wameuwawa katika shambulio hilo la kijeshi, ikiwa ni pamoja na wanajeshi wawili wa Lebanon.

Serikali ya mjini Beirut inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi inalishutumu kundi la Fath al – Islam, ambalo inasema lina mahusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaeda , unaojaribu kuiyumbisha nchi hiyo. Waziri wa mawasiliano ya simu Marwan Hamadeh ameiambia televisheni ya Deutsche Welle kuwa jeshi la Lebanon limeamua kuchukua hatua madhubuti dhidi ya wapiganaji hao.

Jeshi hilo limewataka wapiganaji hao kujisalimisha na wakaazi wa Nahr al-Bared kutowapa hifadhi.