1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Maelfu ya watu wamiminika kwa kumbukumbu ya mauaji ya Hariri

14 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCSC

Maelfu ya Walebanon wamekusanyika katika uwanja ulio katikati mwa Beirut hii leo kwa kukumbuku ya mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri, aliyeuwawa kwenye shambulio la bomu.

Serikali imetuma maofisa wa usalama kuzuia kuzuka machafuko kufuatia mashambulio ya mabomu dhidi ya mabasi ya abiri hapo jana yaliyowaua watu watatu. Waziri mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora pamoja na mkewe ni miongoni mwa viongozi waliofanya maombi katika kaburi la Rafik Hariri mjini Beirut.

Wafuasi kadhaa wa upinzani walipiga kambi kwenye mahema katika uwanja huo kuishinikiza serikali ya waziri mkuu Siniora ijiuzulu. Polisi walitumia magari yasiyoweza kutobolewa na risasi na waya wa seng´eng´e kuwatenganisha wafuasi wa serikali na wa upinzani. Polisi pia waliwapekua watu wote waliokuwa wakiingia kwenye uwanja wa karibu la hayati Rafik Hariri huku helikopta ya jeshi ikiizunguka anga ya uwanja huo.

Serikali inatumai idadi kubwa ya watu waliojitokeza kwa kumbukumbu hiyo itaipa nguvu dhidi ya upinzani unaongozwa na kundi la Hezbollah na kumaliza maandamano ya kila siku ambayo sasa yameingia mwezi wa tatu.