1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Mapigano makali yazuka tena kaskazini mwa Lebanon

18 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBqd

Mapigano makali yamezuka mapema leo kwenye kambi ya wakimbizi ya Nahr el Bared kaskazini mwa Lebanon.

Vikosi vya jeshi la Lebanon vimewashambulia kwa mabomu wanamgambo wanaoungwa mkono na kundi la Alqaeda walio ndani ya kambi hiyo.

Wakisaidiwa na vifaru na silaha nzito, wanajeshi wa Lebanon wamezishambulia pia ngome za wanamgambo hao ndani ya kambi ya Nahr el Bared iliyo katika viunga vya mji wa bandari ya Tripoli, huku mapambano yakiingia wiki yake ya tano.

Walioshuhudia wanasema mashambulio ya mabomu ya jeshi la Lebanon yemesababisha moshi mweupe na mweusi kutanda kwenye anga ya eneo hilo na kuzusha moto kwenye majengo kadhaa ndani ya kambi hiyo ya wakimbizi.

Kwenye mapambano ya jana wanajeshi wa Lebanon waliyaharibu makao makuu ya wanamgambo wa Ftah al Islam yaliyokuwa kwenye mpaka wa kambi hiyo, lakini kiongozi wa kundi hilo, Shaker Youssef al Absi na wapambe wake wakuu hawajulikani waliko mpaka sasa.

Mapigano baina ya wanamgambo wa Fatah al Islam na wanajeshi wa Lebanon yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 150 tangu yalipoanza mnamo tarehe 20 mwezi uliopita.