1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT : Mbunge mashuhuri auwawa katika mripuko

14 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBru

Mripuko wa bomu magharibi mwa mji mkuu wa Beirut Lebanone umeuwa watu tisa na kujeruhi wengine kadhaa hapo jana.

Mbunge mashuhuri anayeipinga Syria Walid Eido ameuwawa katika mripuko huo ambao pia imeripotiwa kumuuwa mwanawe wa kiume na walinzi wake wawili.Huu ni mripuko wa sita kutokea katika mji mkuu wa Beirut katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.

Ingawa bado haijulikani nani aliehusika na mripuko huo kiongozi wa kundi la wabunge walio wengi katika bunge la Lebanone Saad Hariri ameilaumu Syria kwa mauaji ya mbunge Walid na ameutaka Umoja wa Waarabu kuisusia serikali aliyoita kuwa ya kigaidi ya Syria.

Saad ambaye ni mbunge amesema mauaji hayo yanatokana na wale wale waliohusika na mauaji ya baba yake waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik Hariri katika mripuko wa bomu kwenye gari hapo mwezi wa Februari mwaka 2005.

Bila ya kuitaja kwa jina Syria Saad amesema ni utawala huo wa kigaidi unaokiuka haki ya Lebanone kujitawala,kudhoofisha usalama wake na kuwauwa wanasiasa wake.

Saad amekuwa akiishutumu Syria hadharani kwa mauaji ya baba yake.