1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

BEIRUT: Watu takriban 60 wajeruhiwa kwenye maandamano

23 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCYS

Maelfu ya Walebanon wamefanya maandamano makubwa katika barabara za mjini Beirut hii leo. Barabara, maduka, biashara na shule zilifungwa wakati maelfu ya waandamanaji walipotii amri ya kundi la Hezbollah kufanya maandamano. Duru za polisi zinasema watu takriban 60 wamejeruhiwa.

Kuanzia leo asubuhi barabara zilifungwa mjini Beirut na sehemu nyengine nchini Lebanon kutumia matairi ya magari na takataka. Maandamano hayo ni hatua ya hivi punde ya kundi la Hezbollah kutaka kuiondoa madarakani serikali ya waziri mkuu Fouad Siniora inayoegemea mataifa ya magharibi na uchaguzi wa mapema uitishwe nchini humo.

Waziri Siniora amekataa masharti ya kundi hilo. Fouad Siniora ameshindwa kusafiri kwenda mjini Paris Ufaransa kuhudhuria mkutano wa wahisani wa Lebanon uliopangwa kufanyika keshokutwa Alhamisi.

´Lebanon ina watu wazuri lakini ni ndogo na uchumi wake haujaimarika. Na sasa inajiandaa kwa mkutano wa mataifa 40 utakaoyashirikisha mashirika na makampuni mbalimbali. Yote haya yanakutana kujadili njia za kuisaidia Lebanon.´

Waziri Siniora amesema mkutano wa mjini Paris sio tu kwa faida ya serikali ya sasa ya Lebanon, bali kwa taifa zima kwa jumla.