1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bemba sasa kujibu mashtaka The Hague

Admin.WagnerD19 Novemba 2010

Jumatatu ijayo (22 Novemba 2010), Mahakama ya Kimataifa mjini The Hague inaanza kusikiliza kesi dhidi ya Jean-Pierre Bemba kuhusu ushiriki wake katika uhalifu wa kivita kwenye nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

https://p.dw.com/p/QDnm
Jean-Pierre Bemba akionekana katika Mahakama ya Kimataifa Uhalifu, mjini The Hague, Uholanzi (Picha ya AP/Peter Dejong)
Jean-Pierre Bemba akionekana katika Mahakama ya Kimataifa Uhalifu, mjini The Hague, Uholanzi (Picha ya AP/Peter Dejong)Picha: AP

Tarehe 30 Julai 2006, Jean-Pierre Bemba alikuwa mtu tafauti na alivyo leo. Hapo alikuwa mgonbea urais katika nchi yake ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Alionekana mchangamfu, anayejiamini na mwenye matumaini ya kuwa rais ajaye.

"Nina matumaini ya kuungwa mkono na Wakongo, kwamba wanaweza kubadilisha hali ya mambo na kujitengenezea falsafa mpya kwa kuiweka serikali mpya nchini Kongo." Ndivyo alivyowaambia waandishi wa habari, baada ya kupiga kura yake.

Lakini mambo yakamgeukia. Mshindani wake, Joseph Kabila, ndiye aliyeibuka mshindi. Bemba akahofia maisha yake. Mwezi Aprili 2007 akakimbilia Ureno. Mwezi Mei 2008 akakamatwa na askari wa Ubelgiji, na mwezi Juni mwaka huo huo akajikuta yuko kwenye mahabusu ya The Hague.

Jumatatu ya keshokutwa (22 Novemba 2010), Bemba atasimama kwenye kizimba cha Mahakama ya Kimataifa, ambako waendesha mashtaka wanamtuhumu kwa uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu. Uhalifu huo unajumuisha mauaji, ubakaji na utekaji nyara. Anashitakiwa kwa mambo yaliyotendeka katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati baina ya mwezi Oktoba 2002 hadi Machi 2003.

Kwa waathirika wa uhalifu huu, kuanza kwa kesi hii ni mwanzo mzuri. Mwakilishi wao, Marie-Edith Lawson, anasema kwamba hata kama madhara waliyotendewa hayawezi kufutika, bado wanastahiki kuujua ukweli na wawe na uwezekano wa kuusajili ushahidi wao.

"Wakosa lazima waadhibiwe. Hilo ndilo linaloweza kuwaridhisha wahanga."

Jean-Pierre Bemba, siku hizo akiwa mgombea urais wa DRC, akiwapungia mkono wafuasi wake hapo mwaka 2006 (Picha ya AP/Schalk van Zuydam)
Jean-Pierre Bemba, siku hizo akiwa mgombea urais wa DRC, akiwapungia mkono wafuasi wake hapo mwaka 2006 (Picha ya AP/Schalk van Zuydam)Picha: AP

Lakini kwa wafuasi wa Bemba, makamo huyu wa rais wa zamani ni mtu safi. Kwao wao, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa, Luis Moreno-Ocampo, ni muongo. Vile vile wanaamini kwamba wakati Bemba alipokuwa kiongozi wa kundi la Ukombozi wa Kongo, MLC, hakuhusika na maafa yaliyokuwa yakitokea Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Hivyo ndivyo anavyohoji mwanasheria wake, Aimé Kilolo, ambaye anasema pana tafauti baina ya kuwa kiongozi wa kijeshi na kuwa kiongozi wa MLC, ambayo baina ya Oktoba 2002 na Machi 2003, ilikaa mjini Bangui.

"Kwa hili, msimamo wetu uko wazi: Jamhuri ya Afrika ya Kati iliomba wapiganaji kutoka MLC. Watu hawa wangelikuwa wanagharamiwa na kupokea amri kutoka serikali ya huko. Kwa hivyo, haiwezekani kuhukumu kwamba Jean-Pierre Bemba alikuwa kiongozi kwenye eneo hilo."

Lakini hoja hii inapingwa vikali na Lawson, ambaye anasema ukweli kuwa Bemba hakuwepo kwenye eneo uhalifu ulipokuwa unatokea, haimaanishi kwamba hahusiki, maana ni yeye (Bemba) aliyelikabidhi bendera hilo kundi la wapiganaji wake waliokwenda kufanya uhalifu.

Na kwa hakika, jambo hili ndilo linaloifanya kesi hii ya Bemba kuwa ya aina yake. Hakuna anayejua kesi hii itachukuwa muda gani, maana matayarisho yake tu yamechukua miaka miwili. Bado kuna majibizano makubwa ya hoja kati ya upande wa mashtaka na utetezi na bado haijajuilikana kwamba Bemba atakutwa mkosa au mtu safi!

Mwandishi: Mohammed Khelef/Konstanze von Kotze/ZPR

Mhariri: Othman, Miraji